Logarusic alisema ili kikosi chake kiweze kurejea katika ushindani atawatema kwenye programu zake wachezaji hao ambao amewakuta wameshasajiliwa.
Hata hivyo, kocha huyo raia wa Croatia, hakuwa tayari kuwataja majina nyota hao wanaomwangusha katika mechi za ligi na kusababisha timu yao kuendelea kukaa kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu.
Baadhi ya wachezaji ambao wanadaiwa wamekuwa wakifanya 'ndivyo sivyo' na kumchanganya kocha huyo ni pamoja na Betram Mwombeki, Uhuru Selemani na Zahor Pazi ambaye Jumamosi jijini Mbeya aliingia kuchuka nafasi ya Haroun Chanongo katika dakika ya 54 na kupoteza nafasi zaidi ya tatu za kuifungia Simba na kufanya mechi hiyo imalizike kwa sare ya 1-1.
Simba yenye pointi 31 huku ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, jana jioni ilianza mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi, Sinza kwa ajili ya kujiandaa na mechi yake itakayofanyika Jumapili, Februari 23, mwaka huu dhidi ya JKT Ruvu.
Yanga ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa ndio mabingwa watetezi wa ligi wakati Azam ndio vinara wakiwa na pointi 36 wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 35 na Mbeya City wakiwa na pointi 34 ni watatu.