Kikosi
cha watu 27 wakiwemo wachezaji na benchi la ufundi cha timu ya Taifa ya
vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) kinatarajia
kuondoka keshokutwa (Aprili 3 mwaka huu) kwenda Nairobi, Kenya.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam leo (Aprili 1 mwaka huu), Kocha Simkoko amesema wachezaji wake
wapo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, na nia ni kupata matokeo mazuri
kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini wiki tatu baadaye.
Kikosi cha Ngorongoro Heroes chenye
wachezaji 20 na viongozi saba kitaondoka saa 4.30 asubuhi kwa ndege ya
Kenya Airways. Msafara wa timu hiyo utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Vijana.
Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi
Abdoulkarim Twagiramukiza, Ambroise Hakizimana, Raymond Bwiliza na Louis
Hakizimana wote kutoka Rwanda wakati Kamishna ni Maxwell Mtonga wa
Malawi.
Ngorongoro Heroes itaagwa kesho (Aprili 2 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF.
MIKOA KUMI YATUMA WAWAKILISHI WAKE RCL
Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kumi vimewasilisha majina ya mabingwa wao watakaoshiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Mabingwa hao ni Arusha (AFC),
Kilimanjaro (Panone FC), Lindi (Kariakoo SC), Manyara (Tanzanite SC),
Mara (JKT Rwamukoma), Morogoro (Volcano FC), Mtwara (Pachoto Shooting
Stars), Pwani (Kiluvya United), Shinyanga (Bulyanhulu FC), Singida
(Singida United) na Tanga (African Sports).
Mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa
wake ni Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa, Kagera, Katavi, Kigoma,
Mbeya, Morogoro, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Simiyu na Tabora wakati mikoa ya
Dodoma na Mwanza imeomba kuongezewa muda kutokana na sababu mbalimbali.
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliagiza kuwa mikoa yote iwe imemaliza
ligi na kuwasilisha jina la bingwa wake Machi 30 mwaka huu.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)