Tuesday, September 23, 2014

KIONGERA NJE KUIKOSA YANGA KATIKA MTANANGE WATANI WA JADI OCT 12 MWAKA HUU.

MSHAMBULIAJI Mahiri Wa Simba Mkenya, Paul Raphael Kiongera yupo katika hatari ya kukosa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga SC Oktoba 12, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hiyo inafuatia kuumia katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Jumapili Uwanja wa Taifa, Simba SC ikilazimishwa sare ya 2-2 na Coastal Union, licha ya kuongoza kwa 2-0 hadi mapumziko.

Kiongera alitokea benchi dakika ya 67, lakini dakika mbili kabla ya mpira kumalizika  alimpisha Amri Kiemba baada ya kuumia, kufuatia kugongana na kipa wa Coastal Union, Shaaban Kado.

Kiongera ameumia goti ambapo leo alikuwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa vipimo, ila inasemekana mchezaji huyo ana maumivu sugu ya goti hilo baada ya kuumia awali kwao, Kenya.
Taarifa za awali zinasema Kiongera anaweza kuwa nje ya Uwanja kwa muda wa kati ya wiki sita hadi miezi miwili kabla ya kuanza mazoezi mepesi, maana yake hataweza kucheza Oktoba 12 pambano la watani.

Baada ya taarifa hiyo kuna hali ya wasiwasi ndani ya Simba SC kwamba huenda wameingia mkenge’ kumsajili Mkenya huyo bila kumfanyia vipimo vya afya, kufuatia habari kwamba ana maumivu sugu ya goti.