Friday, November 7, 2014

UKATILI KWA WATOTO BADO TATIZO KATIKA JAMII YA KITANZANIA.

MTOTO aliyefahamika kwa jina moja la Rehema Matola mwenye umri wa miaka sita, mkazi wa Airport jijini Mbeya amefanyiwa vitendo vya ukatili na mama yake wa kambo, ambae hakuweza kufahamika.
Vitendo anavyodaiwa kufanyiwa mtoto huyo ni kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake, kisha kung’olewa jino, kujeruhiwa eneo la mdomo na mguuni, pamoja na kuumizwa sehemu zake za siri hali iliyopelekea mwili wake kudhoofu.
Mtoto huyo ambaye mama yake mzazi alikwishafariki dunia amedai kuwa amekuwa akipigwa mara kwa mara na mama yake wa kambo na wakati mwingine na baba yake hali inayomsababishia  majeraha na kisha kumwacha ndani bila kumpatia matibabu mpaka pale majirani walipobaini na kutoa taarifa kwenye uongozi wa serikali za mitaa.
Nae Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Airport,kata ya Ileya bi, Rehema Mohamed amelaani tukio hilo na kusisitiza kuwa sio la mara ya kwanza na ameziomba mamlaka husika kupita mitaani na kwa ajili ya kutoa elimu.
Hata hivyo juhudi za kumtafuta mtuhumiwa huyo hazikuzaa matunda kwani amekimbia mara baada ya tukio hilo.