Tuesday, June 25, 2013

EFF-LAMTIMUA KIBARUA KATIBU MKUU WAKE""

SHIRIKISHO la Soka la Ethiopia-EFF limemtimua kibarua katibu mkuu wake baada ya kukiri kumtumia mchezaji kimakosa katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 hatua ambayo inaweza kuigharimu timu nchi hiyo kukatwa alama tatu. Kamati ya Utendaji ya EFF ilipiga kura za kumtimua katibu huyo aitwaye Ashenafi Ejigu lakini walipinga barua ya kujiuzulu kwa makamu wa rais wa shirikisho hilo Berhanu Kebede ambaye ndiye alikuwa akilaumiwa kutokana na mkanganyiko huo. Baadhi ya wajumbe na waandishi wa habari za michezo waliokuwepo katika mkutano huo walikuwa wakitaka uongozi mzima wa shirikisho hilo ujiuzulu kwa kile walichokiita uzembe. Rais wa EFF, Sahilu Gebremariam alikiri kuwa suala hilo ni la kizembe na wanapaswa wote kujiuzulu na kudai kuwa atafanya hivyo katika mkutano mkuu utakaofanyika Septemba mwaka huu. Akihojiwa kuhusiana na suala la kumchezasha mchezaji aliyepewa kadi mbili za njano kocha wa Ethiopia Sewnet Bishaw alijitetea kuwa anapokuwa uwanjani huwa hatumii karatasi na kalamu anachofanya yeye ni kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.

YANGA WAJIPNGA NA MECHI ZA KIRAFIKI

Mabingwa wa soka Tanzania Bara , Afrika Mashariki na Kati, Klabu ya Dar Young Africans watacheza mechi za kirafiki  dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda Julai 6 na 7, mwaka huu katika sehemu ya ziara yake ya kulitembeza Kombe lake la ubingwa wa Ligi Kuu mikoa ya kanda ya Ziwa inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)  kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kaimu katibu mkuu wa Yanga Lawrence Mwalusako , Yanga maarufu kama Kwalalumpa Malysia itaondoka Dar es Salaam Julai 5, siku mbili tu baada ya kuanza  mazoezi Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam kuelekea Mwanza tayari kwa mchezo wa kwanza dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati, Uwanja wa CCM Kirumba, Julai 6.
Baada ya kipute hicho, Julai 7, timu hizo ambazo zimewahi kufundishwa na kocha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Raoul Jean Pierre Shungu kwa wakati tofauti na kwa mafanikio, zitarudiana kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
“Yanga tuna mipango mingi sana, bahati mbaya tumeshindwa kwenda Sudan kutetea ubingwa wetu wa Kagame, lakini bado tuna michuano mikubwa barani Afrika, ikiwa ni heshima kwa mashabiki wetu na wanachama wanaotuunga mkono, ni nafasi yao kuliona taji letu la ligi msimu uliopita, tutapita mikoani na kushangilia pamoja”. Alisema Mwalusako. Baada ya hapo , Yanga SC wataelekea mjini Tabora, kucheza mechi nyingine na wenyeji, Rhino FC waliopanda Ligi Kuu msimu huu Julai 11, mwaka huu Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.
Katika ziara hizo, Yanga watatembeza Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu, walilolitwaa kwa mara ya 24 msimu huu kwenye mitaa mbalimbali kushangilia na mashabiki wao. 
Yanga SC, imekuwa na mafanikio makubwa tangu ianze kudhaminiwa na TBL mnamo 2008, ikitwaa jumla ya mataji sita katika kipindi hicho, yakiwemo mawili ya Kagame, 2011 na 2012 na manne ya Ligi Kuu Bara, 2008, 2009, 2011 na 2013. Agosti 2, mwaka 2011, TBL ilisaini Mkataba wa udhamini na Yanga wa miaka minne sawa na kwa watani wao pia, Simba SC.
Katika mkataba huo mpya, uliotiwa saini kwenye hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es Salaam, TBL iliongeza dau la fedha za mishahara kwa wachezaji kutoka Sh. Milioni 16 hadi Milioni 25 kwa mwezi, ikaongeza basi moja kubwa, Yutong lenye uwezo wa kubeba abiria 54 na fedha kwa ajili ya kugharamia mikutano ya wanachama ya kila mwaka Sh. Milioni 20 kugharamia tamasha la mwaka la klabu na vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh. Milioni 35 kila msimu.
Yanga pia inapewa bonasi ya Sh. Milioni 25 ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara au Milioni 15, ikishika nafasi ya pili katika Mkataba huo wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 5 tangu Agosti 8, mwaka huu hadi Julai 31, mwaka 2016.

TETESI ZA MASTAA NA KITUO CHA REDIO CHA NAPOLI MARTE-CAVANI

KITUO cha Redio cha Napoli, Marte kimetangaza kuwa dau la Pauni Milioni 49.3 limetolewa na Chelsea kwa ajili ya mshambuliaji  Edinson Cavani ambaye muda wote anampasua kichwa mmiliki wa klabu ya Chelsea Bilionea Roman Abramovich mwenye lengo la kuimarisha kikosi chake chini ya kocha Jose Mourinho.
Katika taarifa ya jana usiku, Radio Marte ilitangaza: “Tumepokea taarifa kutoka ofisini kwa vyanzo vya kuaminika kwamba, Napoli imekubaliana dili la kuiuzia Chelsea Cavani.

Kitu moto: Chelsea sasa ipo katika nafasi ya kumnasa Edinson Cavani
“Rafa Benitez pia amebariki, lakini kabla ya kutangaza rasmi, Napoli inataka kupata mshambuliaji atakayeziba pengo la Il Matador.
“Aurelio De Laurentiis”, klabu itasomba kiasi cha Euro Milioni 58, sawa na dili la Ezequiel Lavezzi kwenda PSG mwaka jana.
“Mchezaji huyo atajiingizia mshahara wa Euro Milioni 8.5 kwa msimu pamoja na haki za picha,”. Habari zimevuja kama kwamba Cavani ametangaza anataka kukutana uso kwa uso na Rais, Aurelio de Laurentiis na kuna taarifa kwamba Manchester United nayo imo kwenye mbio hizo. 
Mshambuliaji huyo wa Uruguayna baba yake awali walionyesha nia ya kutaka kwenda Real Madrid. Klabu hiyo ya Hispani iliwasiliana na Napoli, lakini sasa itabidi waipiku ofa iliyotolewa na Chelsea.
                                  Hata Man United na PSG pia zinamtaka Cavani

Monday, June 24, 2013

RAMBIRAMBI MSIBA WA MATHIAS KISSA

Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Cosmopolitan na Taifa Stars, Mathias Kissa (84) kilichotokea leo alfajiri (Juni 24 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani enzi zake, Kissa akiwa na timu ya Tabora alitamba katika michuano ya Kombe la Taifa wakati huo ikiitwa Sunlight Cup. Alikuwa akicheza katika nafasi ya ulinzi.

Baadaye alijiunga na Cosmoplitan ya Dar es Salaam, na pia kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ambapo enzi zake akiwa na wachezaji kama Yunge Mwanansali wakiiwakilisha Tanganyika na baadaye Tanzania Bara walitamba katika michuano ya Kombe la Chalenji wakati huo ikiitwa Gossage, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

Kissa ambaye alipata tuzo ya mchezaji bora wa karne kwa upande wa Tanzania, tuzo inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) alikuwa ndiye mchezaji msomi kupita wote wakati akichezea timu ya Taifa akiwa amehitimu elimu ya Darasa la Kumi.

Kwa mujibu wa binti yake, Erica, marehemu ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi (stroke) alioupata miaka mitano iliyopita, na kisukari. Baadaye alipata kidonda ambacho ndicho kilichosababisha kifo chake.

Msiba uko nyumbani kwa marahemu, Masaki, Mtaa wa Ruvu karibu na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST). Maziko yatafanyika keshokutwa, Jumatano (Juni 26 mwaka huu) kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kisa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Cosmopolitan na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Kisa mahali pema peponi. Amina

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

TYSON AFUZU MBIO ZA DUNIA BAADA YA KUTUMIA SEKUNDE 19.74

Mwanariadha nyota wa Marekani, Tyson Gay amefanikiwa kufuzu kushiriki mbio za mita 200 za duniani zitakazofanyika jijini Moscow kwa kutumia muda wa sekunde 19.74 ambao ni muda wa haraka zaidi kwa mwaka huu. Gay ambaye ni bingwa wa dunia wa mwaka 2007, sasa atachuana na mwanariadha mwenye kasi zaidi duniani kutoka Jamaica, Usain Bolt katika mbio za mita 100 na 200 kwenye mashindano ya dunia yatakayofanyika jijini Moscow, Urusi Agosti mwaka huu. Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka aliwashinda Isiah Young aliyeshika nafasi ya pili na Curtis Mitchell alishika nafasi ya tatu. Kwa upnde wa wanawake mwanadada nyota katika mbio fupi kutoka Marekani Allyson Felix alishindwa kutamba kwenye mbio za mita 200 baada kushindwa na Kimberlyn Duncan.

ARSHAVIN SASA AFIKIRIA KURUDI ALIPOTOKA KISOKA CLUB YA "ZSP"

Baada ya kuitumikia Arsenal kwa muda wa miaka mitano nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Urussi, Andrei Arshavin anategemewa kukamilisha taratibu za kurejea klabu yake ya zamani ya Zenit Saint PetersburgKlabu hiyo ndio ilimuwezesha arshavin mwenye miaka 32 akiwa kinda kabla ya Arsenal kumuona na kumyakuwa. aidha Arshavin ambaye alikaa Zenit kwa mkopo kwa muda wakati wa msimu wa pili wa 2011-2012 kwa sasa yuko huru baada kuachwa na Arsenal mwishoni mwa msimu huu. hata hivyo nyotahuyo ni moja kati ya wachezaji waliokuwemo katika kikosi cha Zenit kilichonyakuwa taji la Europa League mwaka 2008 na pia katika kikosi cha Urusi kkilichoshiriki michuano ya Ulaya 2008 kabla ya kwenda Arsenal.

SUAREZ AWEKA REKODI YA KUWA MCHEZAJI ALITUPIA MABAO MENGI NA TIMU YA TAIFA.

MSHAMBULIAJI Mahiri wa kimataifa wa Uruguay, Luis Suarez ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo wa Kombe la Shirikisho ambao waliibigiza Tahiti kwa mabao 8-1. Nyota anayekipiga katika klabu ya Liverpool ya Uingereza alifunga bao lake la 35 na 36 na kumpita mchezaji mwenzake wa nchi hiyo Diego Forlan wakati timu hiyo ilipokata tiketi ya kucheza nusu fainali dhidi ya wenyeji Brazil Jumatano huko Belo Horizonte. Mabao mengine ya Uruguay katika mchezo huo yalifungwa na Abel Hernandez aliyefunga manne huku Diego Perez na Nicolas Lodeiro wakifunga bao moja kila mmoja na kupelekea Tahiti chovu kuaga mashindano hayo na mzigo wa magoli 24 ya kufungwa. Uruguay ilitinga uwanjani bila kuwaanzisha nyota wake kama Forlan, Edinson Cavani na Suarez ambaye aliingia kipindi cha pili kwa ajili ya kuwapumzisha kwa ajili ya mchezo wa Jumatano.