Tuesday, February 18, 2014

LOGARUSIC NITAFANYA KWELI MSIMBAZI KUHUSU WACHEZAJI"L

Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, amesema matokeo mabaya ya timu hiyo katika mechi za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara ambayo iko hatua ya lala salama yanatokana na kuwa na baadhi ya wachezaji wasio na viwango 'mizigo'.

Logarusic alisema ili kikosi chake kiweze kurejea katika ushindani atawatema kwenye programu zake wachezaji hao ambao amewakuta wameshasajiliwa.

Hata hivyo, kocha huyo raia wa Croatia, hakuwa tayari kuwataja majina nyota hao wanaomwangusha katika mechi za ligi na kusababisha timu yao kuendelea kukaa kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu.

Baadhi ya wachezaji ambao wanadaiwa wamekuwa wakifanya 'ndivyo sivyo' na kumchanganya kocha huyo ni pamoja na Betram Mwombeki, Uhuru Selemani na Zahor Pazi ambaye Jumamosi jijini Mbeya aliingia kuchuka nafasi ya Haroun Chanongo katika dakika ya 54 na kupoteza nafasi zaidi ya tatu za kuifungia Simba na kufanya mechi hiyo imalizike kwa sare ya 1-1.

Baada ya mechi ya ugenini dhidi ya Mbeya City, Logarusic, alisema kwamba ubingwa wa ligi bado uko wazi na ili Simba iweze kurejesha matumaini ya kumaliza katika nafasi za juu ni lazima mabingwa watetezi, Yanga, Azam na Mbeya City zilizoko juu yake zifanye vibaya kwenye mechi zao.

Simba yenye pointi 31 huku ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, jana jioni ilianza mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi, Sinza kwa ajili ya kujiandaa na mechi yake itakayofanyika Jumapili, Februari 23, mwaka huu dhidi ya JKT Ruvu.

Yanga ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa ndio mabingwa watetezi wa ligi wakati Azam ndio vinara wakiwa na pointi 36 wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 35 na Mbeya City wakiwa na pointi 34 ni watatu.

MNYIKA: WADAU WASHIRIKISHWE KUTUNGA KANUNI ZA BUNGE LA KATIBA.

Mbunge  wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amesema atawasilisha mapendekezo ya kutaka ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba ibadilishwe, ili wadau washirikishwe kwenye mchakato wa kutunga kanuni za Bunge hilo.

Mnyika alisema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.

Alisema  ratiba iliyotolewa inaonyesha kwamba baada ya kusomwa kwa tangazo la kuitisha Bunge hilo na uchaguzi wa mwenyekiti wa muda, kazi ya kutunga kanuni itaanza.

Mnyika alisema kanuni ndiyo msingi wa kufikia mwafaka wa kuboresha rasimu ya Katiba badala ya kuchakachua na kwamaba ili zisitungwe kanuni mbovu ipo haja ya wadau wote wanaohusika na mchakato wa Katiba mpya ndani na nje ya Bunge kushiriki.

“Nakusudia kuwasilisha mapendekezo kwamba ratiba  ya Bunge ifanyiwe mabadiliko ili kuwapo na kikao cha kusikiliza umma (Public hearing), juu ya kanuni hizo ili mawazo ya wadau yazingatiwe katika maandaluzi ya kanuni kabla ya Bunge kupitisha azimio la kuridhia kanuni hizo,” alisema Mnyika.

Aidha, alisema atawasiliana na Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi au Mwenyekiti wa muda atakayechaguliwa ili kanuni zisitolewe nakala kwa wajumbe hao pekee, bali iwekwe kwenye tovuti za Bunge, za Baraza la Wawakilishi, za serikali ili ziwe wazi kwa wadau wazijadili.
Alisema kanuni za kawaida za Bunge zimekuwa zikitoa mamlaka makubwa sana kwa maspika kwa kiwango, ambacho wamekuwa wakifanya maamuzi mabovu na kusababisha vurugu.

“Ni lazima Bunge la Katiba liwe na kanuni, ambazo zinatoa mamlaka zaidi kwa wajumbe na pia kuweka msingi wa kujenga mwafaka zaidi wa kitaifa kwa kuwa Katiba ni maridhiano ya wananchi na siyo ushindani wa vyama au makundi mbalimbali,” alisema Mnyika.

Alisema wajumbe ni wawakilishi tu wa kuwezesha mwafaka huo kufikiwa na kanuni ni nyenzo ya kuongoza majadiliano ya kufikia maridhiano kwa kuzingatia maoni ya wananchi na maslahi ya umma.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, leo wajumbe hao watakuwa na jukumu la kuandaa na kupitisha kanuni za Bunge Maalumu.
Chanzo:Nipashe.

RATIBA KAMILI RAUNDI YA KWANZA LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Yanga SC (Tanzania) Vs Al Ahly (Misri)
Berekum Chelsea (Ghana) Vs Ahli Benghazi (Libya)
Gor Mahia (Kenya) Vs Esperance (Tunisia)
Enyimba (Nigeria) Vs AS Real (Mali)
Astres de Douala (Cameroon) Vs TP Mazembe (DRC)
B.Y.C (Liberia) Vs Sewe Sport (Ivory Coast)
Dedebit (Ethiopia) Vs CS Sfaxien (Tunisia)
Horoya (Guinea) Vs Raja Casablanca (Morocco)
Flambeau de l’Est (Burundi) Vs Coton Sport (Cameroon)
Entente Setif (Algeria) Vs ASFA Yennenga (Burkina Faso)
Stade Malien (Mali) Vs El Hilal (Sudan)
AC Leopards (Congo) Vs Primeiro de Agosto (Angola)
Kaizer Chiefs (Afrika Kusini) Vs Liga Muçulmana (Msumbiji)
Dynamos FC (Zimbabwe) Vs AS Vita Club (DRC)
Zamalek (Misri) Vs Kabuscorp (Angola)
Nkana (Zambia) Vs Kampala City Council (Uganda) 
(Mechi za kwanza zitachezwa kati ya Februari 28 na Machi 2 
na marudiano zitachezwa kati ya Machi 7 na 9 mwaka huu)

VIDIC WA MAN UNITED AKUBALI KWENDA YAKE ITALY

BEKI Kisiki Nemanja Vidic wa Man united amekubali kujiunga na Inter Milan ya Italia. Nyota huyo wa kimataifa wa Serbia ambaye alitangaza Januari kuamua kuondoka Old Trafford mwishoni mwa msimu huu anatazamiwa kuasaini dili la  mkataba wa miaka miwili ambao utamuwezesha kulipwa kitita cha euri milioni tatu kwa mwaka. Kuna taarifa kuwa Vidic aliwafahamisha viongozi wake wa United kuhusu uamuzi wake wa kukubali kwenda nchini Italia baada ya kufikia makubaliano kwenye mchezo waliotoka sare ya bila ya kufungana na Arsenal katika uwanja wa Emirates Jumatano iliyopita. Ofisa mkuu wa Inter, Piero Ausilio amekuwa na mawasiliano ya karibu na nyota huyo toka Januari alipotangaza kutaka kuondoka. Toka atangaze kuondoka Vidic amekuwa akiwendwa na vilabu mbalimbali huku Monaco ya Ufaransa na Galatasaray ya Uturuki zikiwa mojawapo lakini nyota huyo ameamua kwenda Italia. Vidic alijiunga na United akitokea klabu ya Spartak Moscow ya Urusi mwaka 2006 na amefanikiwa kushinda mataji matano ya Ligi Kuu na moja la Ligi ya Mabingwa barani ULaya katika kipindi cha miaka nane aliyokaa Old Trafford.

Monday, February 17, 2014

WENGER AMJIBU MBWATUKAJI MOURINHO

Kocha wa Klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amefafanua kauli ya Jose Mourinho kumuita mtaalamu wa kushindwa kuwa ni kauli ya kijinga na iliyokosa heshima. Kauli ya hiyo ya Mourinho aliitoa kujibu kauli iliyotolewa na Wenger kuwa baadhi ya mameneja wa timu za Ligi Kuu nchini Uingereza wanadai kuwa hawana mpango na taji hilo msimu huu kutokana na uoga wao. Akihojiwa Wenger amesema hataki kuingia katika vita ya maneno na Mourinho lakini anadhani kauli yake ni aibu kwa timu yake ya Chelsea kuliko ilivyo kwake. Wenger amesema asingependa kuzungumzia kauli za kijinga na zilizokosa heshima kwasababu huwa hapendi kumzungumzia Mourinho katika mikutano yake na waandishi wa habari na hatakuja kufanya hivyo. Kocha huyo alikipongeza kikosi chake kwa kucheza vizuri katika mchezo dhidi ya Liverpool ambao uliwawezesha kukata tiketi ya robo fainali ya Kombe la FA kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

KAKA ASEMA NI MCHEZA NA MCHEZAJI BORA CRISTIANO RONALDO

KIUNGO Mahiri wa klabu ya AC Milan ya Italia, Kaka amebainisha kuwa Lionel Messi na Zinedine Zidane ni wachezaji bora aliokutana nao na kudai kuwa Cristiano Ronaldo ndio mchezaji bora kabisa kuwahi kucheza naye. Kiungo huyo wa kimataifa wa Brazil, amewahi kukutana na Messi mara kadhaa wakati akicheza Real Madrid ambako alikuwa akicheza sambamba na Ronaldo. Kaka aliandika katika ukurasa rasmi wa twitter wa Milan wakati akijibu maswali ya mashabiki ambapo amesema wachezaji bora aliowahi kucheza dhidi yao ni Zidane na Messi huku akimtaja Ronaldo kama mchezaji bora aliyewahi kucheza naye. Kaka pia alimtaja Paulo Maldini kama beki bora kabisa duniani kuwahi kucheza naye kabla hajaondoka Milan kwenda Madrid.

TPS KUWAWEZESHA WASICHANA WALIOKOSA FURSA

Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), imeahidi kuchangia Sh. milioni 1.7 kwa ajili ya kitengo cha wasichana waliokosa fursa.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa TPSF, Godfrey Simbeye, aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kitengo hicho kilichopo chini ya usimamizi wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara, kazi za mikono na nguo. (Tahowete).

Simbeye alisema atakwenda kuwaombea fedha hizo TPSF ili kuwasaidia wasichana hao watano katika shule ya ushonaji na kuongeza kuwa wajasiriamali wangewezeshwa kwa kuwa wakifanya biashara wanaweza na bila kuwezeshwa hawawezi kufanya jambo lolote.

Aidha alisema serikali ina mpango wa kuanzisha miradi ambayo wanataka iwawezeshe wanawake,.

Mwenyekiti wa Tawohate, Anna Matinde, alisema chama hicho kinasaidia jamii hasa wasichana wanaomaliza masomo na kukosa ajira, pamoja na wale wanaonyanyasika kijamii kwa kuanzisha miradi ambayo wasichana hao waliokatiza masomo waweze kuendelea na masomo.
Chanzo: Nipashe