Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
aliyekuwa Katibu Mkuu wake (wakati huo ikiitwa FAT), Kanali mstaafu Ali
Hassan Mwanakatwe kilichotokea leo asubuhi (Juni 7 mwaka huu) katika
Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa binti wa marehemu, Sophia,
baba yake alianguka bafuni nyumbani kwake Mbezi Beach ambapo
alikimbizwa katika Hospitali ya Lugalo ambapo ndipo umauti ulipomfika
wakati madaktari wakimpatia matibabu.
Kanali Mwanakatwe alichaguliwa kuwa
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) katika uchaguzi
uliofanyika mwaka 1993 mjini Kibaha mkoani Pwani.
Baada ya kuondoka FAT, aligombea nafasi
ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
na kufanikiwa kushinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1997.
Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira
wa miguu nchini na Afrika kwa ujumla kwani, Kanali Mwanakatwen enzi za
uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi, na mkufunzi wa utawala
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Pia aliwahi kuwa Kamishna
wa CAF.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu
Kanali Mwanakatwe, DRFA, na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na
kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha
msiba huo mzito.
Taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa
na familia yake nyumbani kwake Mbezi Beach karibu na hoteli ya Giraffe
wakati ndugu wakisubiriwa kutoka mikoani. TFF tunasubiri taratibu hizo
ili tujipange jinsi ya kushiriki katika msiba huo.
Sisi sote ni waja wake Mola. Hakika kwake tutarejea.