
Benchi la Ufundi la Taifa Stars pamoja
na wachezaji kesho (Julai 19
mwaka huu) saa 5 asubuhi watakuwa na mkutano na waandishi wa habari
kwenye hoteli ya Protea
Courtyard iliyopo Upanga
Seaview jijini Dar es Salaam.
Naye mchezaji Mwinyi Kazimoto amewasili leo 1.30 asubuhi kwa ndege ya Qatar
Airways
kutoka Qatar ambapo anacheza mpira wa miguu katika klabu ya Al Markhiya
ya huko. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga
kambi katika hoteli ya Protea Courtyard.
SERENGETI BOYS MORALI JUU
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari amesema morali ya
wachezaji wake ipo juu kwa ajili ya mechi dhidi ya Afrika Kusini
(Amajimbos) itakayochezwa kesho (Julai 18 mwaka huu).
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa
vijana wenye umri chini ya miaka 17 itafanyika kwenye Uwanja wa Azam
Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF
jijini Dar es Salaam leo, Kocha Hababuu amesema nia ya kikosi chake ni
kuhakikisha wanafika kwenye fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani
nchini Niger.

“Tunaiheshimu Afrika Kusini, lakini hatuiogopi. Morali ya wachezaji
ipo juu na wanajiamini. Kimsingi wanajua kuwa hii ndiyo njia ya wao
kutokea kwenye mpira wa miguu, kwa hiyo lengo ni kushinda,” amesema
Kocha Hababuu.
Naye Kocha wa Afrika Kusini, Molefi Ntseki amesema anaziheshimu timu za
Tanzania,
na changamoto aliyonayo ni kuhakikisha kuwa anashinda mechi hiyo kwani
mara ya mwisho kwa timu yake kushiriki fainali za Afrika ilikuwa miaka
sita iliyopita.
Kiingilio katika mechi hiyo ni sh. 2,000 na tiketi zitapatikana uwanjani kwenye magari maalumu.
MSUMBIJI KUTUA MCHANA DAR
Timu ya Taifa ya Msumbiji (Mambas) inawasili Dar es Salaam kesho
(Julai 18 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika dhidi ya
Taifa Stars itakayochezwa Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mambas itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) saa 7.30 mchana kwa ndege ya LAM ikiwa na

msafara wa watu 37 ambapo kati ya hao, 25 ni wachezaji.
Wachezaji kwenye msafara huo ni Almiro Lobo, Apson Manjate, Bone
Mario Uaferro, Dario Ivan Khan, Edson Sitoe, Eduardo Jumisse, Gelicio
Aurelio Banze, Helder Pelembe, Josemar Machaisse, Elias Pelembe, Isac
Carvalho na Jeffrey Constatino.
Wengine ni Manuel Fernandes, Manuel Uetimane, Mario Sinamunda, Momed
Hagi, Reginaldo Fait, Reinoldo Mandava, Ricardo Campos, Saddan Guambe,
Simao
Mate Junior, Soares Victor Soares, Stelio Ernesto, Vando Justino na Zainadine Junior.
Timu hiyo itafikia kwenye hoteli ya Accomondia, na itaondoka Jumapili
mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mahmoud Ashour.
LINA KESSY AUTEULIWA KUWA OFISA MICHEZO AU
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Lina Kessy ameteuliwa kuwa Ofisa Michezo wa Umoja wa Afrika
(AU).
Uteuzi huo umefanywa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Nkozasana
Dlamini-Zuma, na Lina atatumikia nafasi hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu
katika makao makuu ya AU yaliyopo
Addis Ababa, Ethiopia.
Lina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake
Tanzania (TWFA) amewashukuru wote ambao kwa michango yao ya hali na
mali imemwezesha kufika hapo.
Ameishukuru TFF kwa kumlea na kumjenga. Shukrani nyingine amezitoa
kwa Serikali kupitia Kurugenzi ya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa
(BMT) na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).
TFF inampongeza kwa uteuzi huo, na tunaamini ataipeperusha vyema
bendera ya Tanzania ikiwemo kuwa chachu ya maendeleo ya michezo kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)