Friday, November 7, 2014

UKATILI KWA WATOTO BADO TATIZO KATIKA JAMII YA KITANZANIA.

MTOTO aliyefahamika kwa jina moja la Rehema Matola mwenye umri wa miaka sita, mkazi wa Airport jijini Mbeya amefanyiwa vitendo vya ukatili na mama yake wa kambo, ambae hakuweza kufahamika.
Vitendo anavyodaiwa kufanyiwa mtoto huyo ni kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake, kisha kung’olewa jino, kujeruhiwa eneo la mdomo na mguuni, pamoja na kuumizwa sehemu zake za siri hali iliyopelekea mwili wake kudhoofu.
Mtoto huyo ambaye mama yake mzazi alikwishafariki dunia amedai kuwa amekuwa akipigwa mara kwa mara na mama yake wa kambo na wakati mwingine na baba yake hali inayomsababishia  majeraha na kisha kumwacha ndani bila kumpatia matibabu mpaka pale majirani walipobaini na kutoa taarifa kwenye uongozi wa serikali za mitaa.
Nae Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Airport,kata ya Ileya bi, Rehema Mohamed amelaani tukio hilo na kusisitiza kuwa sio la mara ya kwanza na ameziomba mamlaka husika kupita mitaani na kwa ajili ya kutoa elimu.
Hata hivyo juhudi za kumtafuta mtuhumiwa huyo hazikuzaa matunda kwani amekimbia mara baada ya tukio hilo.

TFDA:MAMA NTILIE MBEYA WATAKIWA KUBORESHA MAENEO YA KAZI.

MAMLAKA  ya chakula na dawa TFDA, kanda ya nyanda za juu kusini imekiri kuwa mazingira wanayofanyia biashara baadhi ya mamantiliye jijini Mbeya, hayakikidhi viwango vya usafi hali inayoweza kuhatarisha afya za watumiaji wa vyakula.
Hayo yamebainishwa na kaimu meneja wa TFDA, wa kanda hiyo Rodney Analanga wakati akizungumza na Highlands fm radio ofisini kwake.
Analanga amesema kuwa mamlaka hiyo haitasita kuwachukulia hatua za kisheria mama ntiliye ambao hawafuati kanuni za usafi wa chakula ikiwa ni pamoja na kutumia maji safi na vyombo vilivyooshwa na maji safi na salama.
Kauli hiyo imekuja kufuatia Highlands fm, kufanya uchunguzi kwenye mabanda ya mama ntilie katika eneo la Sido jijini Mbeya na kubaini kuwa wafanyabiashara hao hawakidhi viwango vya usafi wa chakula.

VPL:TIKETI ZA ELEKTRONIKI KUTOUZWA KWENYE MAGARI

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea wikiendi hii ambapo tiketi za elektroniki hazitauzwa tena kwenye magari, hivyo washabiki wanunue tiketi hizo kwenye mtandao au kwenye maduka ya CRDB Fahari Huduma.

Kesho (Novemba 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutakuwa na mechi kati ya Yanga na Mgambo Shooting wakati Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi kati ya Azam na Coastal Union. Jumapili ni mechi kati ya Simba na Ruvu Shooting.

Viingilio kwenye mechi za Uwanja wa Taifa ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu, sh. 8,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 (VIP B na C) wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Mechi za Uwanja wa Chamazi kiingilio ni sh. 3,000 kwa sh. 10,000.
Mechi nyingine za VPL kesho ni kati ya Stand United na Mbeya City (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), Mtibwa Sugar na Kagera Sugar (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

Raundi hiyo ya saba itakamilika Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Ndanda kutoka Mtwara.
Wakati huo huo, mchezaji bora wa VPL kwa mwezi Oktoba, Salum Abubakar wa Azam atakabidhiwa zawadi yake kesho (Novemba 8 mwaka huu) kabla ya mechi kati ya Azam na Coastal Union.

Thursday, November 6, 2014

UEFA:BARCA,BAYEN MUNICH,PSG FC PORTO ZATINGA 16 BORA

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya imeendelea tena jana na kushuhudia timu za Barcelona, Bayern Munich, Paris Saint-Germain-PSG na FC Porto nazo zikitinga hatua ya timu 16 bora baada ya kushinda michezo yao. Katika michezo ya michuano hiyo iliyochezwa juzi mabingwa watetezi Real Madrid na Borussia Dortmund nao walitangulia katika hatua hiyo baada ya kushinda mechi zao. Barcelona wao walifanikiwa kusonga mbele baada ya kuitandika Ajax Amsterdam kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na nyota wake Lionel Messi wakati Bayern Munich wao waliichapa kwa mara nyingine AS Roma kwa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Allianz Arena. PSG wao walisonga mbele baada ya kuitandika Apoel kwa bao 1-0 huku Porto nao wakicharuka na kuichapa Athletic Bilbao kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na nyota wa Colombia Jackson Martinez na Mualgeria Yacine Brahimi.
Wiki hii imekuwa mbaya kwa timu za Uingereza kwani baada ya Liverpool kuiweka rehani nafasi yao ya kusonga mbele kwa kufungwa na Madrid kwa bao 1-0 huku Arsenal wakitoa sare nyumbani na Anderlecht, Chelsea nao wameingia katika mkumbo huo baada ya kugawana alama na Maribor kwa kutoka sare ya bao 1-1. Kwa upande wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu hali yao ndio imezidi kuwa mbaya baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya CSKA Moscow ya Urusi katika Uwanja wa Etihad na kuweka matumaini yao ya kusonga mbele katika mashaka.

MESSI AFIKIA REKODI YA RAUL BAO 71 AMBWAGA RONALDO UEFA

Mshambuliaji Mahiri wa Argetina na Barcelona Lionel Messi amefanikiwa kuifikia rekodi ya nyota wa zamani wa Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Raul Gonzalenz alikuwa akishikilia rekodi ya kufunga mabao 71 na kuwa mfungaji mwenye mabao mengi zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Cristiano Ronaldo alionekana ndiye atakuwa wa kwanza kumfikia Raul,lakini mabao mawili aliyofunga Messi wakati Barcelona ikiichalaza Ajax magoli 2-0 kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, yamekwamisha ndoto za Ronaldo.
Wafungaji Bora: wa Kihistoria Uefa.
Lionel Messi: Magoli 71 Mechi 90-Barcelona.
Raul: Magoli 71 Mechi 142-Real Madrid na Shalke 04.
C'Ronaldo: Magoli 70 Mechi 107-Man united na R'Madrid
Ruud van Nistelrooy: Magoli 56 Mechi 73-Psv Eindhoven,Man U na R'Madrid.
Thierry Henry: Magoli 50 Mechi 112-Arsenal,Barca,Los angel marekani.

JESHI LA POLISI MBEYA LAMSHIKILIA MTU MMOJA KWA KUUZA NYAMA YA MBWA

KATIKA tukio la kushangaza mwanaume mmoja amekamatwa na polisi wilaya ya Kyela mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kuuza nyama ya Mbwa.
Mtuhumiwa huyo amefahamika kwa jina la Ahad Jesikaka mwenye umri wa miaka 20, mkazi wa kijiji cha Ngyekye, kata ya Matema, wilayani humo.
Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amesema kuwa amewauzia kitoweo hicho watu wawili.
Amewataja walionunua nyama hiyo ni Enock Nsemwa mwenye miaka 25, na Anyandile Mbwilo mwenye umri wa miaka 29, wote wakazi wa Ngyekye.
Hata hivyo anatoa wito kwa jamii kuwa makini hususuni wanaponunua vyakula ili kujiepusha na madhara ya kiafya.

MWANAFUNZI WA DARASA LA 5 AFARIKI KWA VIBOKO NCHINI KENYA

Mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya msingi ya Kiuu Kenya amefariki dunia baada ya kupigwa na mwalimu wake kwa kufeli somo lake la Kiswahili.
Familia ya mtoto huyo Joseph Waburi mwenye umri wa miaka kumi imesema mtoto huyo alikuwa na nidhamu ya hali ya juu.
Mama wa mwanafunzi huyo Grace Muthoni amesema mtoto wake alienda shule Jumatatu asubuhi na aliporudi alianza kulalamika maumivu ya kichwa na shingo, siku iliyofuatia alimpeleka Zahanati ya Wilaya ya Nyagiti level 4.
Siku ya pili alilazimika kumrudisha Hospitali baada hali yake kuzidi kuwa mbaya daktari akashauri ahamishiwe katika Zahanati ya Muran’ga Level 4 kwa matibabu zaidi wakati akisubiri gari la wagonjwa akafariki dunia.
Mama huyo amesema uchunguzi wa awali unaonyesha mtoto wake alipigwa na Mwalimu na kupata majeraha kichwani na shingoni, mwili wake umehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi kubaini sababu za kifo chake.
Mwalimu anayedaiwa kumpiga Mwanafunzi huyo alikimbia kujificha shimoni baada ya kusikia taarifa za kifo, huku Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Joseph Mwenda akikanusha uvumi kwamba mtoto huyo alifia shuleni.