Unyenyekevu {kuwa na kiasi }
Mwaka 2007 Agosti 14,
nilisimamishwa Kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kosa la kumwita Waziri wa Nishati
na Madini Bwana Nazir Karamagi muongo. Kiukweli nilisimamishwa kwa sababu
nilitoa hoja Bungeni iliyoiabisha Serikali - Hoja ya Buzwagi.
Wananchi walikasirishwa na
kitendo hicho na kuamua kunipokea kwa maandamano makubwa sana nilipoingia
Jijini Dar Es Salaam na kwenye mikoa mingine niliyofanya ziara.
Mawaziri waliotumwa kueleza
maamuzi ya Bunge walizomewa na kumwagiwa mchanga. Mzee Samwel Sitta, Spika wa
Bunge la Tisa, alikuwa anatumiwa sms za 'kifedhuli' kwa mujibu wa maneno yake;
nyingine alinitumia kunisihi nizungumze na ' wafuasi' wangu ili waache kufanya
hivyo. Hasira ya Wananchi ilikuwa kubwa sana na ilionekana wazi wazi.
Siku ya tarehe 19 Agosti
nilitoka Dodoma kuelekea Dar Es Salaam. Kabla sijafika Chalinze ya Dodoma
alinipigia simu kaka yangu Abdurahman Mbamba, akanisihi sana kuwa mnyenyekevu
kwa maongezi yangu. Nasaha hizi kwa kweli zinaniongoza mpaka leo hii. Kwenye mafanikio
ya jambo fulani au hata kutofanikiwa, nakumbuka maneno ya Abdurahman Mbamba.
Nilipokuwa nahutubia
Jangwani siku hiyo, niliongea kwa ufupi sana. Watu wakapiga kelele niendelee
kuongea. Ningeweza kuongea nitakavyo maana ndio nilikuwa ' star' wa nyakati.
Mshale wa nasaha zile ukanichoma ' kuwa mnyenyekevu '!
Nikawaambia wananchi '
siwezi kuendelea kuongea, nina Viongozi wangu hapa'. Alikuwapo Mheshimiwa
Freeman Mbowe, Dkt. Willibrod Slaa, Mheshimiwa Augustine Mrema, Maalim Seif
Sharif Hamad, ndg. Ibrahim Lipumba na Bwana James Mbatia.
Kwa unyenyekevu nilishuka
jukwaani na kutoa nafasi kwa Viongozi kuzungumza. Watu walitaka na ningetaka
ningeendelea lakini la hasha, nilikataa.
Rais aliunda Kamati ya
kupitia Mikataba ya Madini. Aliniteua katika Kamati ile iliyoongozwa na Jaji
Mark Bomani. Watu wangu wengi ' wa karibu' walinisihi nisikubali kuingia kwenye
kamati. Mmoja alithubutu kuniambia ' snubb him' akimaanisha Rais.
Kwamba ningepata umaarufu zaidi. Ningeweza
kukataa na kuwafurahisha watu waliotaka kumwaibisha Rais. ' kuwa mnyenyekevu'
yakawa ni maneno yananirudia kila wakati.
Hilo na kiu ya kuijua Sekta
ya Madini vilivyo yalinishawishi kukubali uteuzi ule. Walionishawishi kukataa
hawakunisamehe mpaka leo. Utawasikia wakisema ' Kamati ya Bomani haikufanya
lolote'.
Wakati huo huo wanakuwa
mstari wa mbele kufurahia mabadiliko makubwa sana kwenye Sekta ya Madini
ikiwemo kuongezeka Mapato ya kikodi, umiliki wa Serikali kwenye migodi, Madini
ya Vito kuchimbwa na Watanzania pekee na hata kuanza kutozwa kwa Kodi ya
ongezeko la mtaji ( capital gains tax ).
Yote hayo yametokana na
mapendekezo ya Kamati ya Bomani yaliyozaa Sera mpya ya Madini ya mwaka 2009
iliyopelekea Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2010.
Mwaka 2014 tunaufunga kwa
suala la akaunti ya Tegeta Escrow. Bunge lilifanikiwa kupitisha maazimio 8
yaliyowasilishwa Serikalini kwa utekelezaji. Maazimio hayo yalipatikana kwa
maridhiano ya Bunge zima. Ni mafanikio makubwa ambayo yanashawishi wahusika
wakuu kufurahia au hata ku 'claim credit'.
Mbunge mmoja kijana rafiki
yangu kutoka Mkoa wa Arusha akaniambia ' brother this is your resurrection ' na
usiache. Mwandishi mmoja wa gazeti la kila wiki akaniambia ' it's a come back '
na kunitaka nifanye ziara Nchi nzima kuelezea suala hili.
Wenzangu kwenye Siasa
wakaandaa maandamano Jijini Dar ambayo nilikataa. Shemeji yangu mmoja
akaniambia ' kwenye ushindi jua pa kuishia'. Maneno haya hayana tofauti na
nasaha za Abdurahman.
Sasa kuna juhudi kubwa za
kutetea waliotajwa na Taarifa ya Kamati ya PAC. Magazeti, haswa ya Serikali
yamekuwa yakiandika habari zenye mwelekeo wa kutetea.
Ikulu imeagiza Taarifa ya CAG ichapwe kwenye
magazeti, jambo ambalo halijapata kutokea huko nyuma kwani sio mara ya kwanza
PAC kutumia Taarifa ya CAG kuwajibishana.
Makala zinaandikwa
kumshawishi Rais asitekeleze maamuzi ya Bunge. Nasaha za ' know where to stop '
na ' kuwa mnyenyekevu ' zinanivuta na kunishawishi kutosema lolote.
Hekima inataka kumwachia
Mkuu wa Nchi kuamua kwa namna itakavyompendeza. Tumwache aamue. Unyenyekevu
unataka hivyo. Wenye ushawishi tofauti walikuwa na nafasi Bungeni.
Walishindwa ndani ya Baraza
la Taifa. Unyenyekevu ni kwa walioshindwa pia.