Thursday, June 27, 2013

FEDERER ASEMA BADO ATAENDELEA KUCHEZA MCHEZO HUO".

Mchezaji tenesi mahiri wa Switzerland, Roger Federer amesisitiza kuwa bado ataendelea kucheza mchezo huo kwa miaka mingi ijayo pamoja na kutolewa mapema katika michuano ya Wimbledon jana. Nyota huyo ambaye anashika namba tatu katika orodha za ubora duniani amesema hana hofu yoyote pamoja na kutolewa na Sergiy Stakhovisky wa Ukraine katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo. Katika mchezo huo Federer aliburuzwa kwa kufungwa 6-7 7-6 7-5 7-6 na Stakhovsky anayeshika namba 116 katika orodha za ubora duniani. Baadhi ya wadau wa mchezo huo wamekuwa wakihoji kiwango cha Federer mwenye umri wa miaka 31 na kudai kuwa amekwisha lakini mwenye amesisitiza kuwa bado yuko fiti na ataendelea kucheza kwa miaka kadhaa ijayo. Kwa upande wa wanawake mwanadada nyota anayeshika namba mbili kwa ubora kwa upande wanawake Maria Sharapova wa Urusi naye aliyaaga mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha 6-3 6-4 kutoka kwa Michelle Larcher de Brito wa Ureno anayeshika namba 131 katika orodha hizo.

SCOLARI AMEKIRI KUWA TIMUYA BRAZIL BADO HAIKO FITI-DUNIA

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luis Felipe Scolari amekiri kuwa kikosi chake bado hakiwezi kuanza kuweka matumaini ya kutwaa kombe lao la sita la Kombe la Dunia mwaka ujao lakini wamebakisha mechi moja kunyakuwa taji lao la tatu la Kombe la Shirikisho baada ya kuiengua Uruguay katika hatua ya nusu fainali. Scolari amesema anafikiri kikosi hicho kimefikia mahali pazuri lakini bado kuna vitu vingi vya kufanyia marekebisho mpaka kikamilike kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kwasasa wanahamishia nguvu zao katika mchezo wa fainali na baada ya hapo wataangalia mapungufu yalijitokeza ili kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara kitakachoweza kulibakisha Kombe la Dunia nyumbani. Brazil kwasasa wanasubiri mshindi wa nusu fainali nyingine ya michuano hiyo itakayopigwa baadae leo kati ya mabingwa wa Ulaya na Dunia Hispania watakaochuana na Italia.

ABEL NA KISPANG WAJITOA TIMU YA WANARIADHA WA KENYA

BINGWA mara mbili wa dunia mashindano ya mbio ndefu Abel Kirui na mshindi wa medali ya shaba katika michuano ya olimpiki Wilson Kipsang wamejitoa katika timu ya wanariadha ya Kenya itakayoshiriki michuano ya riadha ya dunia itakayofanyika jijini Moscow. Makamu wa rais wa Chama cha Riadha cha nchi hiyo Paul Mutwii amedai kuwa Kurui aliwafahamisha kwamba amejitoa kwasababu ya kusumbuliwa na majeraha wakati Kipsang yeye amewaambia kuwa ana majukumu mengine. Kirui ambaye alishinda taji la dunia la mbio ndefu mwaka 2009 na 2011 amekuwa akisumbuliwa jeraha la kifundo cha mguu wake wa kulia na anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita. Kuziba nafasi hizo Mutwii amesema wamewaita Mike Kipyego ambaye alishinda mbio za marathon jijini Tokyo mwaka jana, Bernard Kipyego mshindi wa medali ya fedha mbio za nusu marathon 2009 na bingwa wa mbio za marathoni za Paris Peter Some. Kikosi cha mwisho kitakachokwenda Moscow kitatajwa mwezi ujao baada ya kufanyika mbioza mchujo.

JUVESTUS YATANGAZA RASMI KUMSAJILI TEVEZ

KLABU ya Juventus ya Italia jana ilimtangaza rasmi kumsajili mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Argentina, Carlos Tevez kutoka timu ya Manchester City kwa mkataba wa miaka mitatu. Taarifa zinadai kuwa klabu yenye maskani yake katika jiji la Turin wamelipa kiasi cha paundi milioni 10 kwa nyota huyo mwenye umri wamiaka 29. Lakini Tevez atatakiwa kumaliza adhabu yake ya kutumikia jamii kwa saa 250 ili kuondoka jijini London salama na kuepuka kuburuzwa tena mahakamani. Tevez alikatisha likizo yake huko Amerika Kusini na kupanda ndege kuelekea Italia jana lakini pia atatakiwa kumaliza adhabu yake aliyopewa na mahakama ya Macclefield April mwaka huu kwa kuendesha huku akiwa amefungiwa kufanya hivyo.

Tuesday, June 25, 2013

VALCKE-ASEMA BRAZIL NDIO MAHALA PA KOMBE LA DUNIA"

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amesema kuwa hawana mpango wa kubadili mahali patakapochezwa michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Valcke alibainisha kwamba michuano hiyo itafanyika nchini Brazil katika miji 12 kama ilivyopangwa na hakuna mpango mwingine wowote wa kuhamisha mashindano hayo kwenda sehemu nyingine. Kauli ya Valcke imekuja kufuatia maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea nchini humo wakati huu wa michuano ya Kombe la Shirikisho wakipinga gharama kubwa za matayarisho ya Kombe la Dunia wakati wananchi wake wana hali duni katika maisha yao ya kawaida. Valcke pia alipinga kauli ya Waziri wa Michezo wa Brazil, Aldo Rebelo aliyekuwa amekaa pembeni yake katika mkutano na waandishi wa habari aliyedai kwamba kuna nchi zimeonyesha nia ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kama Brazil ikijitoa. Katibu mkuu huyo amesema hajapokea ofa yoyote kutoka katika nchi yoyote duniani kutaka kuandaa michuano hiyo ya 2014 na kumuondoa hofu Rebelo ambaye alidai amesoma katika vyombo vya habari kwamba nchi za Marekani, Uingereza, Ujerumani na Japan zinamendea nafasi hiyo.

EFF-LAMTIMUA KIBARUA KATIBU MKUU WAKE""

SHIRIKISHO la Soka la Ethiopia-EFF limemtimua kibarua katibu mkuu wake baada ya kukiri kumtumia mchezaji kimakosa katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 hatua ambayo inaweza kuigharimu timu nchi hiyo kukatwa alama tatu. Kamati ya Utendaji ya EFF ilipiga kura za kumtimua katibu huyo aitwaye Ashenafi Ejigu lakini walipinga barua ya kujiuzulu kwa makamu wa rais wa shirikisho hilo Berhanu Kebede ambaye ndiye alikuwa akilaumiwa kutokana na mkanganyiko huo. Baadhi ya wajumbe na waandishi wa habari za michezo waliokuwepo katika mkutano huo walikuwa wakitaka uongozi mzima wa shirikisho hilo ujiuzulu kwa kile walichokiita uzembe. Rais wa EFF, Sahilu Gebremariam alikiri kuwa suala hilo ni la kizembe na wanapaswa wote kujiuzulu na kudai kuwa atafanya hivyo katika mkutano mkuu utakaofanyika Septemba mwaka huu. Akihojiwa kuhusiana na suala la kumchezasha mchezaji aliyepewa kadi mbili za njano kocha wa Ethiopia Sewnet Bishaw alijitetea kuwa anapokuwa uwanjani huwa hatumii karatasi na kalamu anachofanya yeye ni kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.

YANGA WAJIPNGA NA MECHI ZA KIRAFIKI

Mabingwa wa soka Tanzania Bara , Afrika Mashariki na Kati, Klabu ya Dar Young Africans watacheza mechi za kirafiki  dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda Julai 6 na 7, mwaka huu katika sehemu ya ziara yake ya kulitembeza Kombe lake la ubingwa wa Ligi Kuu mikoa ya kanda ya Ziwa inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)  kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kaimu katibu mkuu wa Yanga Lawrence Mwalusako , Yanga maarufu kama Kwalalumpa Malysia itaondoka Dar es Salaam Julai 5, siku mbili tu baada ya kuanza  mazoezi Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam kuelekea Mwanza tayari kwa mchezo wa kwanza dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati, Uwanja wa CCM Kirumba, Julai 6.
Baada ya kipute hicho, Julai 7, timu hizo ambazo zimewahi kufundishwa na kocha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Raoul Jean Pierre Shungu kwa wakati tofauti na kwa mafanikio, zitarudiana kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
“Yanga tuna mipango mingi sana, bahati mbaya tumeshindwa kwenda Sudan kutetea ubingwa wetu wa Kagame, lakini bado tuna michuano mikubwa barani Afrika, ikiwa ni heshima kwa mashabiki wetu na wanachama wanaotuunga mkono, ni nafasi yao kuliona taji letu la ligi msimu uliopita, tutapita mikoani na kushangilia pamoja”. Alisema Mwalusako. Baada ya hapo , Yanga SC wataelekea mjini Tabora, kucheza mechi nyingine na wenyeji, Rhino FC waliopanda Ligi Kuu msimu huu Julai 11, mwaka huu Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.
Katika ziara hizo, Yanga watatembeza Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu, walilolitwaa kwa mara ya 24 msimu huu kwenye mitaa mbalimbali kushangilia na mashabiki wao. 
Yanga SC, imekuwa na mafanikio makubwa tangu ianze kudhaminiwa na TBL mnamo 2008, ikitwaa jumla ya mataji sita katika kipindi hicho, yakiwemo mawili ya Kagame, 2011 na 2012 na manne ya Ligi Kuu Bara, 2008, 2009, 2011 na 2013. Agosti 2, mwaka 2011, TBL ilisaini Mkataba wa udhamini na Yanga wa miaka minne sawa na kwa watani wao pia, Simba SC.
Katika mkataba huo mpya, uliotiwa saini kwenye hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es Salaam, TBL iliongeza dau la fedha za mishahara kwa wachezaji kutoka Sh. Milioni 16 hadi Milioni 25 kwa mwezi, ikaongeza basi moja kubwa, Yutong lenye uwezo wa kubeba abiria 54 na fedha kwa ajili ya kugharamia mikutano ya wanachama ya kila mwaka Sh. Milioni 20 kugharamia tamasha la mwaka la klabu na vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh. Milioni 35 kila msimu.
Yanga pia inapewa bonasi ya Sh. Milioni 25 ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara au Milioni 15, ikishika nafasi ya pili katika Mkataba huo wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 5 tangu Agosti 8, mwaka huu hadi Julai 31, mwaka 2016.