Friday, July 19, 2013

WENGER ARUSIWA KUONGEZA DAU KUHUSU SUAREZ

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger ameruhusiwa kuongeza ofa kufikia paundi milioni 40 kwa ajili ya kuiwinda saini ya mshambuliaji nyota wa Liverpool Luis Suarez. Mshambulijai huyo wa kimataifa wa Uruguay ndiye mchezaji anayepewa kipaumbele kusajiliwa na Arsenal msimu huu wa majira ya kiangazi ambapo tayari ofa yao ya kwanza ya paundi milioni 30 ilikataliwa na klabu hiyo.  
Mapema wiki hii kulikuwa na tetesi kuwa Arsenal walianzisha mazungumzo na maofisa wa Liverpool kwa kutoa ofa ya paundi milioni 35 lakini nayo ilikataliwa na kuweka wazi kuwa kiasi hicho hakikutosha. Lakini ofa mpya ya paundi milioni 40 inatarajiwa kutikisa mkataba wa Suarez huku wakala wake akidai kuwa ofa hiyo inashawishi hivyo Liverpool wanatakiwa kuisikiliza.

DAVID MOYES ASISITIZA KUHUSU ROONEY-USAJILI

KOCHA wa klabu ya Manchester United, David Moyes kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa Wayne Rooney hawezi kuuzwa baada ya Chelsea kudai kuwa mshambuliaji wa kimataifa wa Uingereza ndio chaguo lao katika kipindi hiki cha usajili majira ya kiangazi. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Sydney, Australia katika ziara yao ya kujiandaa na msimu mpya, Moyes amesema msimamo wa klabu kuhusiana na mustakabali wa nyota huyo bado haujabadilika. Akitupiwa swali lingine kuhusiana na suala ofa iliyotolewa na United kwa ajili ya kumnasa kiungo wa Barcelona, Cesc Fabregas, Moyes amesema hajajua suala hilo linaendeleaje lakini anategemea katika siku mbili zijazo atafahamishwa na maofisa wa United maendeleo yake. Ofa ya kwanza ya meneja mpya wa Chelsea Jose Mourinho kutaka kumsajili nyota huyo tayari imekataliwa na United lakini klabu hiyo bado imeendelea kufuatilia nyendo za nyota huyo.

MBUYU TWITE "MAJERUHI KUIKOSA URA'

Beki mahiri mwenye nguvu na kasi Mbuyi Twite ataikosa mechi ya keshokutwa wakati Yanga itakapowavaa URA, timu inayomilikiwa na kampuni ya watoza kodi ya mapato ya Uganda.

URA itakuwa nchini kucheza mechi mbili za kirafiki, ikianza na Simba kesho kabla ya kuivaa Yanga, keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Twite amesema ataikosa mechi hiyo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti ingawa amekuwa akifanya mazoezi taratibu.

Awali Yanga ilikuwa icheze mechi ya kirafiki dhidi ya 3 Pillars ya Nigeria, jana lakini ikagundulika timmu hiyo ilikuwa bagumashi kupita kiasi.

TFF ikapoga stop mchezo huo kwa kuwa Wanigeria hao walikuwa wameokotana lakini walitaka kucheza na mabingwa wa Tanzania.

TFF YAIPIGA STOPU TIMU ‘FEKI’ TOKA NIGERIA!!


KATIBU MKUU wa TFF, Angetilie Osiah, amesema wamefuta Mechi za Klabu kutoka Nigeria, FC 3 Pillars, walizokuwa wacheze Nchini baada ya Shirikisho la Soka la Nigeria, NFF, kusema haijui lolote kuhusu Timu hiyo na Ziara yake.

Kwa mujibu wa Osiah, imebidi TFF waifute Ziara hiyo ya Klabu hiyo ya Nigeria kwa sababu Kanuni za FIFA haziruhusu Timu kucheza nje ya Nchi zao bila Kibali toka kwa Mamlaka ya Soka ya Nchini kwao.

Vile vile TFF imesema FC 3 Pillars haijapandishwa Daraja kucheza Ligi Kuu ya Nigeria, NPL [Nigeria Premier League] kama vile tamko la Waandaaji wa Ziara yao Nchini, SportLink International, walivyodai kwenye Matangazo yao.

Jana FC 3 Pillars ilikuwa icheze na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam na pia Timu hiyo ilipangiwa kucheza na Coastal Union na Mbeya City, ambayo Msimu huu unaokuja itacheza Ligi Kuu Vodacom baada ya kupanda Daraja.

Licha ya kuifuta Ziara ya FC 3 Pillars, pia Katibu Mkuu wa TFF, Angetiilie Osiah, alibainisha kuwa hata hao Waandaaji, SportLink International, hawajasaliwa na FIFA kwa ajili ya kuandaa Mechi za Kimataifa kama vile taratibu zinavyotaka.

Akiongeza, Osiah alivitaka Vyama vya Soka vya Mikoa viwe waangalifu wasidanganywe na Wajanja wanaoleta Timu toka nje bila ya kufuata taratibu zilizowekwa.

MAELEZO YA SHUKURANI YA MWENYEKITI ALIYEMALIZA MUDA WAKE WA KAMATI YA UCHAGUZI YA TFF

1.Kama wote tunavyofahamu jana uongozi wangu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ulifikia tamati kama mlivyotangaziwa na Rais wa TFF. Kwa heshima kubwa naomba kutumia fursa hii kuwashukuru viongozi na wadau wa soka kwa ushirikiano mkubwa nilioupata kutoka kwao wakati nikitekeleza majukumu mbalimbali ya TFF.
 2. Kwa kushirikiana na viongozi wa mpira wa miguu katika TFF na mikoa yote Tanzania Bara, pamoja na wadau wa soka, nimepata fursa kulitumikia soka la nchi yetu kwa nafasi mbalimbali. Kwa pamoja tumetekeleza majukumu ya ujenzi wa misingi ya uongozi bora katika TFF na wanachama wake.
 3.Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF:
(i)kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, (Jan 2005 - Jan 2007). Nawashukuru pia wajumbe wa Kamati hiyo chini ya Mhe. Said El-Maamry kwa kunichagua kuwa Katibu wa Kamati hiyo. Ushirikiano mlionipatia ulioniwezesha kulitumikia taifa katika soka na kwa pamoja kurejesha nidhamu kwa kiwango kikubwa. (ii)kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu, iliyochunguza mkasa wa timu yetu ya Taifa ya wachezaji wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) mwezi Juni 2005. Nawashukuru wajumbe wa kamati  hiyo chini ya Dr. Hamad Ndee Mkuu wa Idara ya Michezo ya Chuo kikuu cha Dar es salaam, kwa kunichagua kuwa Katibu wa kamati hiyo iliyoandaa taratibu za mashindano ya vijana  ambazo ni msingi  wa mashindano ya vijana wa umri chini ya miaka 17  hapa nchini. 
(iii)kwa kuniteua kuwa Mjumbe wa Kamati Maalumu iliyotayarisha Programu ya kuendeleza Timu ya Taifa kwa kipindi cha miezi 15 (April 2006 hadi Juni 2007). Progamu iliyochangia Tanzania kiinua kiwango cha ubora wa soka kutoka nafasi ya 165 duniani mwezi Februari 2006 hadi nafasi ya 89 mwezi Desemba 2007.
 (iv)kwa kunipa fursa ya kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu ya kuboresha mapato ya TFF mwaka 2009. Nikiwa mjumbe na Katibu wa Kamati hiyo nilipata ushurikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa soka nchini  na nje ya nchi.  Nina imani kuwa TFF itakamilisha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati na ya wadau wa soka ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia tiketi za elektroniki.
 (v)kwa kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF  kwa  vipindi viwili; Februari 2009 - Machi 2011 na kuniteua tena kuiongoza Kamati hiyo kwa kipindi cha pili Machi 2011 hadi jana tarehe 18 Julai 2013. Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF kwa imani kubwa iliyoonyesha kwangu na wanakamati wenzangu.
4.Nawashukuru wajumbe wote wa wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa ushirikiano mkubwa mliotoa kwangu na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kushiriki kwa amani na utulivu na kuzingatia Katiba za vyama vyenu, Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi na hivyo kufanikisha zoezi la chaguzi za viongozi katika wilaya zote na Mikoa yote ya Tanzania Bara na hivyo kuwezesha kuwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu, ambao  katika kikao chake cha kwanza baada ya chaguzi hizo kimefanya jambo la kihistoria kuweka nguzo za  Mwenendo, Maadili  na Miiko ya uongozi wa soka la nchi yetu. Nilifarijika kuwa sehemu ya Mkutano Mkuu huo nikiwa mwalikwa.
5.Nawashukuru viongozi na wafanyakazi wote wa Sekretarieti ya TFF, wajumbe wa Kamati zote za TFF, Wajumbe wa Kamati zote za Uchaguzi za wanachama wa TFF na wanachama wao, kwa ushirikiano mkubwa na wa dhati uliowezesha kuwatumikia wadau wa soka kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
6.Nawashukuru sana wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ushirikiano niliopata kutoka kwao kwa muda tuliofanya kazi pamoja. Si jambo rahisi kusimamia chaguzi za mikoa yote na klabu zenye wanachama za Ligi Kuu, hata hivyo kwa kushirikiana na wadau mbalimali wa soka ambao nachukua fursa hii kuwashukuru, kwa pamoja tumeweza kutimiza jukumu hilo kikamilifu.  
7.Nawashukuru sana Wandishi na Wahariri wa habari za michezo na pia Wahariri Watendaji wa vyombo vya habari, kwa ushirikiano mzuri nanyi, ushirikiano na uhusiano wa uwazi ambao haukuwa na mikwaruzo ya aina yoyote kwa kipindi chote (Jan 2005-Jul 2013) tulichoshirikiana kwa pamoja kulitumikia soka la nchi yetu.
8.Namshukuru sana Rais wa TFF Ndg. Leodegar Tenga kwa imani kubwa aliyonayo kwangu na kwa wanakamati niliokuwa nao katika kutekeleza majukumu ya umma. Miaka ishirini na tisa (29) iliyopita nilipata fursa ya kufanya kazi ya mpira miguu kwa mara ya kwanza na Ndg. Tenga, nikiwa nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Chuo kikuu cha Dar es salaam, Desemba 1984, wakati Ndg. Tenga alipojitolea kuifundisha timu ya Chuo Kikuu cha DSM. Tangu wakati huo hadi sasa imani  na  ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya umma niliopata kutoka kwa Ndg. Tenga haujawai kutetereka hata kwa siku moja. Ni faraja kubwa kwangu kufanya kazi hizi za umma chini ya kiongozi anayeheshimika na kuaminika na wadau wa soka hapa nchini, Afrika Mashariki na Kati, Afrika na familia ya soka Duniani kwa ujumla. 
9.Mwisho, kwa viongozi na wadau wote wa mpira wa miguu, nawashukuru na nawatakia kheri, baraka  na mafanikio katika Uchaguzi Mkuu wa TFF na  ujenzi wa  soka la nchi yetu..
 Asanteni.
 Deogratias J. Lyatto
19 Julai 2013, Dar es salaam, Tanzania.

Wednesday, July 17, 2013

NURI SAHIN APATA FARAJA KWA USAJILI WA BORUSSIA DORTMUND"

Kiungo nyota wa Club ya Borussia Dortmund, Nuri Sahin ameonyesha furaha na shauku kwa usajili uliofanywa na klabu hiyo huku akiwa na matumaini ya kupiku utawala wa wapinzani wao Bayern Munich katika soka la Ujerumani. 
Ujio wa wachezaji kama Pierre-Emerick Aubameyang, Henrikh Mikhitaryan na Sokratis Papastathopoulous katika kikosi cha Jurgen Klopp kunategemewa kuisimamisha Bayern kurudia mafanikio ya kushinda mataji yote matatu nchini humo.  
Sahin, ambaye amebakisha miezi 12 ya mkopo kutoka klabu ya Real Madrid ana matumaini usajili huo unaweza kuwaongezea nguvu ili kupambana na Bayern ambao kwasasa wametawala soka la nchi hiyo. Dortmund walitolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na DFB-Pokal na Bayern msimu uliopita huku pia wakimaliza nyuma kwa alama 25 mbele ya Bayern ambayo ndio walikuwa mabingwa wa Bundesliga.

LIGI KUU NCHINI MISRI YAWEKWA KAPUNI KWA SABABU ZA KIUSALAMA"

Ligi Kuu ya kandanda nchini Misri imesimamishwa kwasababu za kiusalama kufuatia jeshi la nchi hiyo kumuondoa rais Mohamed Mursi madarakani mapma mwezi huu. Shirikisho la Soka la nchi hiyo lilitangaza rasmi kusitisha msimu wa ligi wa 2012-2013 huku kukiwa kumebaki mzunguko mmoja msimu kumalizika na timu nne kucheza hatua ya mtoano kwa ajili ya kumpata bingwa. Kwa zaidi ya wiki mbili toka jeshi limuondoe Mursi baada ya maandamano makubwa ya kumpinga, kumekuwa na vurugu huku watu zaidi ya saba wakiripotiwa kufa katika mapigano baina waislamu waliokuwa upande wa Mursi na wengine waliokuwa wakimpinga rais huyo. Hii ni mara ya pili katia kipindi cha miaka miwili ligi kusimamishwa katikati ya msimu baada ya mapema mwaka jana ligi hiyo kusitishwa tena kutokana na vurugu zilizotokea Port Said na kusababisha vifo vya mashabiki wapatao 74.