Wednesday, August 14, 2013

SUAREZ AJA NA MTAZAMO MPYA KUHUSU KUBAKIA LIVERPOOL

Mshambuliaji mahiri wa club ya Liverpool, Luis Suarez amebadili mawazo kuhusu mustakabali wake na kusisitiza kuwa ameamua kubakia Anfield. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay amekuwa akitaka kuondoka Uingereza kutokana na kuchoshwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo lakini Liverpool walikuwa hawako tayari kumuachia nyota huyo. Arsenal ambao ushiriki wao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ulionyesha kumvutia Suarez, walijitahidi kujaribu kumsajili nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 kwa kutoa ofa ya paundi milioni 42 ambayo ingevunja rekodi yao ya usajili lakini walikataliwa. Akihojiwa jijini Tokyo akiwa katika majukumu ya timu yake ya taifa, Suarez amebainisha kuwa ameamua kubakia kwa ajili ya mashabiki wa klabu hiyo ambao wameonyesha mapenzi makubwa kwake.

YANGA YAINGIA KAMBINI KUJINOA DHIDI YA AZAM NGAO YA JAMII



MABINGWA wa ligi kuu msimu uliopita  YANGA SC wameingia kambini makao makuu ya klabu yao, Jangwani, Dar es Salaam maarufu kama Jangwani City kujiandaa na mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Jijini.
Wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu, wakiingia kambini Jangwani, wapinzani wao Azam FC waliorejea jana kutoka Afrika Kusini walipoweka kambi ya takriban wiki mbili, wamefikia kwenye makao yao makuu, Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mchezo huo wa kuashiria kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara umeteka hisia za wengi na kila timu inaonekana kupania kushinda ili kuwasha taa za kijani kuelekea mbio za ubingwa.
Yanga iliifunga Azam FC katika mechi zote tatu za msimu uliopita walizokutana, hivyo kulipa kisasi cha kufungwa na timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa mara nne msimu uliotangulia katika mashindano yote waliyokutana.  
Katika kujiandaa na msimu, Yanga SC walicheza mechi saba na kushinda tatu, kufungwa moja na sare tatu.
Walizifunga Mtibwa Sugar 3-1, SC Villa ya Uganda 4-1 na 3Pillars ya Nigeria 1-0, na kutoa sare ya 1-1 na Express, 2-2 na URA zote za Uganda na 0-0 na Rhino FC mjini Tabora, wakati walifungwa 2-1 na Express ya mjini Shinyanga.
Kwa upande wa washindi wa pili wa Ligi Kuu, Azam kabla ya kwenda Afrika Kusini walicheza mechi nne na kushinda tatu, 1-0 na komabini ya JKT, 4-0 na African Lyon na 5-1 Ashanti United. Azam pia ilicheza mechi tatu na kikosi chake cha pili, Azam Akademi na kushinda zote, 1-0 mara mbili na 2-1 mara moja.
Na ikiwa Afrika Kusini, ilicheza mechi nne na kufungwa tatu na kushinda moja- ilifungwa 3-0 na Kaizer Chiefs, 2-1 na Orlando Pirates na 1-0 na Moroka Swallows, wakati yenyewe ilishinda 1-0 dhidi ya Mamelodi Sundowns.


UCHAGUZI TFF KUFANYIKA OKTOBA 18

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa tangazo la uchaguzi wa Kamati ya mpya ya Utendaji ambao utafanyika Oktoba 20 mwaka huu. Pia Kamati hiyo imetoa tangazo za uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPL Board) ambao utafanyika Oktoba 18 mwaka huu.

Akitangaza mchakato huo wa uchaguzi leo (Agosti 14 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hamidu Mbwezeleni amesema nafasi zitakazogombewa kwa upande wa TFF ni Rais, Makamu wa Rais na wajumbe 13 wa Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.

Fomu kwa wagombea zitatolewa kuanzia Agosti 16 mwaka huu kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 kamili jioni kwenye ofizi za TFF. Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Agosti 20 mwaka huu. Fomu kwa nafasi ya Rais ni sh. 500,000, Makamu wa Rais ni sh. 300,000 wakati wajumbe ni sh. 200,000.

Mbwezeleni amesema kwa wale ambao walilipia fomu katika mchakato uliofutwa na wanakusudia kugombea nafasi zilezile walizolipia, hawatalipia tena ada ya fomu husika bali watatakiwa kuambatanisha risiti za malipo wakati wa kurudisha fomu za maombi hayo ili kuthibitisha malipo yao.

Kwa upande wa uchaguzi wa TPL Board, fomu zitaanza kutolewa Agosti 16 hadi 20 mwaka huu, na nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ambapo ada ni sh. 200,000 wakati wajumbe wa Bodi ada ni sh. 100,000.

KAMATI YA SHERIA SASA KUPITIA USAJILI IJUMAA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyokuwa ikutane jana (Agosti 13 mwaka huu) na leo (Agosti 14 mwaka huu) kupitia usajili wa wachezaji kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza sasa itakutana keshokutwa (Agosti 16 mwaka huu) saa 4 asubuhi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Alex Mgongolwa amepanga tarehe hiyo mpya baada ya kikao cha jana kushindwa kupata akidi. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ina wajumbe saba, na ili kikao kiweze kufanyika ni lazima wapatikane wajumbe kuanzia wanne.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

WILAYA YA KORONGWE YAZIDI KUTAKATA KIMICHEZO


TIMU ya Kandanda ya wilaya ya Korogwe leo imetawadhwa kuwa mabingwa wapya wa Mashindano ya Vijana ya Copa Coca Cola ngazi ya mkoa baada ya kufanikiwa kuitandika Muheza mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Mkwakwani mjini hapa.

Mchezo huo ambao ulianza majira ya saa nane mchana ulikuwa mkali na wenye upinzani wa hali ya juu kutokana na timu zote kushambuliana kwa zamu na kuonyesha kandanda nzuri na la kuvutia ambapo hadi timu zote zinakwenda mapumziko,Korogwe walikuwa wakiongoza bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo timu zote ziliingia uwanjani hapo zikiwa na hari ya mchezo baada ya kufanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji wake.

Mabao ya Korogwe yalifungwa na Erick Msagati ambaye alipachika mabao yote kwenye mchezo huo ambao ulikuwa wa aina yake.

SCOLARI ANENA KUHUSU MCHEZAJI NYOTA MESSI

Luis Felipe Scolari kocha wa timu ya taifa ya Brazil,  ametabiri kuwa nyota wa Barcelona Lionel Messi ataendelea kuwa mchezaji bora duniani kwa kipindi cha miaka mingine miwili zaidi. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina ameshinda tuzo nne mfululizo za Ballon d’Or na Scolari bado anaamini kuna vitu vingi vinakuja kutoka kwa nyota huyo mwenye miaka 26 kabla ya umri haujaanza kutafuna kiwango chake. 

Scolari pia alimsifu mchezaji huyo kwa kuwa na kipaji cha hali ya juu na uwezo mkubwa wa kubadili mchezo mwenyewe pindi timu yake inapozidiwa. 

Mbali na Messi, Scolari pia alimnadi mshambuliaji mpya wa Barcelona Neymar kuwa naye atakuja kung’ara kama ilivyo kwa Messi katika kipindi kifupi kijacho. Scolari amesema msimu huu utakuwa muhimu kwa Neymar kwa ajili ya kusoma na kuyazoea mazingira mapya ya Ulaya lakini hana shaka kwamba atachukua kipindi kifupi kuzoea hali hilo na kufanya maajabu kama ilivyokuwa Brazil.

Tuesday, August 13, 2013

ARSENAL YAFIKIA ASILIMIA 99 KUMNASA GUSTAVO

Kiungo mahiri wa kimataifa wa Brazil, Luiz Gustavo anatarajiwa kukubali uhamisho wake kwenda Arsenal ili aweze kucheza zaidi katika kikosi cha kwanza kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil. Kiungo huyo mkabaji wa Bayern Munich ambaye amejikuta akishindwa kupata namba ya moja kwa moja katika kikosi cha kwanza anakaribia kukamilisha usajili wake wa paundi milioni 14 kwenda Emirates wiki hii. Gustavo anaamini kuwa nafasi yake itazidi kuwa finyu chini ya kocha mpya Pep Guardiola ambaye ameonyesha kumtumia sasa Javi Martinez ambaye naye anacheza nafasi hiyo ndio maana anaona uhamisho wake kwenda Arsenal unaweza kumsadia. Akihojiwa jijini Basel kabla ya mchezo wa kirafikiwa kimataifa baina ya Brazil na Switzerland kesho, Gustavo amesema mkataba wake na Bayern unamalizika 2015 lakini ni muhimu kwake kucheza katika kikosi cha kwanza ili aweze kuitwa katika timu ya taifa.

NASRI AOMBA RADHI KUHUSU TABIA YAKE YA LAKINI ASEMA HAJAUWA MTU

Kiungo nyota wa kimataifa wa Ufaransa, Samir Nasri ameomba radhi kwa tabia yake lakini amesisitiza kuwa hajaua mtu hivyo anapaswa kupewa nafasi nyingine ya kujirekebisha. Kiungo huyo anayecheza katika klabu ya Manchester City alifungiwa mechi tatu na Shirikisho la Soka la Ufaransa kufuatia kumtukana mwandishi katika michuano ya Ulaya 2012 na hajaitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo toka kipindi hiko. Hatahivyo Nasri sasa yuko tayari kurejea katika mchezo wa kirafiki kati ya Ufaransa na Ubelgiji baada ya kocha Didier Deschamps kuridhishwa na tabia ya mchezaji huyo. Nasri mwenye umri wa miaka 26 aliomba radhi kwa tukio alilofanya katika michuano hiyo mwaka jana na kudai kuwa angetakiwa kukabiliana na tatizo hilo kwa weledi zaidi kuliko alivyofanya. Nyota aliendelea kudai kuwa anashukuru kupewa nafasi nyingine ya kujirekebisha na ana mategemeo yaliyotokea hayatajirudia kwasababu hivi sasa anajua jinsi gani ya kumudu hasira zake tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma.