Wekundu wa Msimbazi Simba imetua
nanga baada ya kufunga usajili wake wa dirisha dogo kwa kumsaini beki kijana wa
kulia wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hassan Ramadhani Kessy.
Kessy amesaini usiku huu
Mkataba wa miezi 18 baada ya mvutano wa muda mrefu na klabu hiyo juu ya dau.
Zaidi ya mara tatu, Kessy
alikwishakutana mezani na uongozi wa Simba SC bila kufikia maafikiano na baada
ya mvutano huo uliodumu kwa takriban mwezi mzima, leo mambo yameisha.
Kaburu amesema kwamba baada
ya kumpata Kessi wanadhani sasa kikosi chao kimekamilika na wanaelekeza nguvu
zao katika maandalizi kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kessy anakuwa mchezaji wa
nne kusajiliwa na Simba SC katika dirisha dogo, baada ya Waganda beki Juuko
Murushid na washambuliaji Dan Sserunkuma na Simon Sserunkuma.
Murushid amesaini miaka
mitatu, wakati akina Sserunkuma wamesaini miaka miwili kila moja.
Simba SC imewatema Warundi
kiungo Pierre Kwizera na mshambuliaji Amisi Tambwe aliyehamia kwa mahasimu,
Yanga SC baada ya kuwasajili Waganda hao.
Simba SC ililazimika
kuwatema Warundi hao ili kukidhi matakwa ya kanuni ya Usajili ya Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, ya wachezaji watano wa kigeni.
Murushid na akina Sserunkuma
wanaungana na Waganda wenzao, beki Joseph Owino na mshambuliaji Emmanuel Okwi
kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni.