Tuesday, December 16, 2014

SIMBA YAFUNGA USAJILI KWA KUMNASA BEKI WA MTIBWA HASSAN KESSY RAMADHANI

Wekundu wa Msimbazi Simba imetua nanga baada ya kufunga usajili wake wa dirisha dogo kwa kumsaini beki kijana wa kulia wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hassan Ramadhani Kessy.
Kessy amesaini usiku huu Mkataba wa miezi 18 baada ya mvutano wa muda mrefu na klabu hiyo juu ya dau.
Zaidi ya mara tatu, Kessy alikwishakutana mezani na uongozi wa Simba SC bila kufikia maafikiano na baada ya mvutano huo uliodumu kwa takriban mwezi mzima, leo mambo yameisha.
Kaburu amesema kwamba baada ya kumpata Kessi wanadhani sasa kikosi chao kimekamilika na wanaelekeza nguvu zao katika maandalizi kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kessy anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Simba SC katika dirisha dogo, baada ya Waganda beki Juuko Murushid na washambuliaji Dan Sserunkuma na Simon Sserunkuma.
Murushid amesaini miaka mitatu, wakati akina Sserunkuma wamesaini miaka miwili kila moja.
Simba SC imewatema Warundi kiungo Pierre Kwizera na mshambuliaji Amisi Tambwe aliyehamia kwa mahasimu, Yanga SC baada ya kuwasajili Waganda hao.
Simba SC ililazimika kuwatema Warundi hao ili kukidhi matakwa ya kanuni ya Usajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ya wachezaji watano wa kigeni.
Murushid na akina Sserunkuma wanaungana na Waganda wenzao, beki Joseph Owino na mshambuliaji Emmanuel Okwi kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni.