MBIO za mcheza tenisi nyota Andy Murray kufukuzia taji la michuano ya wazi ya Madrid zilisimamishwa na Tomas Berdych katika mchezo wa robo fainali na kumuacha Rafael Nadal kuwa mchezaji pekee anayeshika nafasi za juu kubakia katika michuano hiyo. Murray ambaye anashika namba tatu katika orodha za ubora duniani alishindwa kutamba mbele ya Berdych ambaye ni raia wa Jamhuri ya Czech kwa kukubali kipigo cha 7-6 6-4 huku Nadal naye akipambana na kumfunga Mhispania mwenzake David Ferrer kwa 4-6 7-6 6-0.
Federer ambaye anashika namba mbili kwa ubora alijikuta aking’olewa na Kei Nishikori wa Japan siku moja baada ya kinara wa orodha hizo Novak Djokovic naye kung’olewa na Grigor Dimitrov baada ya kupata maumivu ya kifundo cha mguu wa kulia kwenye mchezo huo.
Nadal sasa atakwaana na Pablo Andujar ambaye naye ni raia wa Hispania baada ya kumuondosha mbabe wa Federer, Nishikori katika hatua ya robo fainali. Vinara wote wanne Djokovic, Federer, Murray na Nadal ambaye anashika na nne kwa ubora watakutana tena katika michuano ya michuano wazi ya Italia wiki mbili zijazo.