
MDHAMINI wa Ligi Kuu Tanzana Bara inayofikia tamati mei 18 mwaka huu, Kampuni ya Vodacom imetangaza kutumia kiasi cha Shilingi Mil 200 kwa ajili ya kutoa zawadi ya fedha taslimu katika ligi inayomalizika mei 18 ambapo sasa Mabingwa wa msimu huu watajipatia Shilingi Milioni 70.
Mbali ya bingwa, Vodacom pia itatoa fedha kwa timu inayomaliza nafasi ya pili, ya tatu na ya nne katika msimamo wa ligi ambazo ni Sh. 35 Milioni, huku Sh. 25 Milioni na Sh. 20 Milioni zote zikiwa na ongezeko ikilinganishwa na zawadi za fedha zilizotolewa katika msimu wa 2012 / 2013.
Zawadi hizo zimetangazwa kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kampuni hiyo kupitia Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom Salum Mwalim, ikiwa ni pamoja na kuainisha zawadi za washindi wa mchezaji mmoja mmoja pamoja na timu iliyoonyesha nidhamu kwa msimu huu.
"Mwaka huu tutatumia kiasi cha Shilingi Milioni 200 kwa ajili ya zawadi za fedha taslimu kwa washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom huku bingwa akinyakua kitita cha Shilingi Milioni 70 ikilinganishwa na Sh 50 Milioni za msimu uliopita." Alisema Mwalim.
Mwalimu amesema lengo la kuongeza zawadi ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya wadhamini wa ligi na wadau wengine wa soka na kwa pamoja kuwa na dhamira ya dhati katika kuendeleza soka nchini.

Aidha, mwamumzi bora na kocha bora kila mmoja atajipatia Shilingi 7,500,000 kila huku timu iliyoongoza kwa nidhamu itapata zawadi ya fedha taslimu ya Shilingi Milioni 15.
"Tumekuwa na msimu mzuri uliojaa ushindani na hamasa, tunatarajia timu zitajipanga zaidi kwa ajili ya msimu ujao na hivyo kuendelea kuipa ubora ligi yetu."Alisema Mwalim huku akiwashukuru wadau wa mpira wa miguu nchini ikiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi, Chama cha Waamuzi(FRAT), Vilabu, wachezaji na kipekee washabiki na kamati ya ligi kuu.
Amesema bila ya ushirikiano wa wadau hao na wengine ikiwemo Serikali, ligi kuu ya Vodacom isingeweza kufikia maendeleo iliyoyafikia katika msimu unaomalizika ambao kwa kiasi kikubwa ulitawaliwa na mpira wa uwanjani na si vinginevyo.