MENEJA wa muda wa
klabu ya Chelsea Rafael Benitez ametanabaisha kuwa anataka kufundisha timu
inayoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kumaliza
kazi yake katika klabu hiyo.
Katika kipindi
kifupi kijacho Benitez ataondoka Stamford Bridge akiwa ameisimamia klabu hiyo
kwa mara ya mwisho Jumamosi iliyopita wakati walipocheza na Manchester City
katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jijini New York Marekani.
Kocha huyo raia wa
Hispania ameiongoza Chelsea kushinda taji la Europa League pamoja na kuisadia
kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kuajiriwa kwa
muda mfupi kuziba nafasi ya Roberto Di Matteo Novemba mwaka jana.
Banitez anaondoka
Chelsea kumpisha Jose Mourinho na kocha huyo sasa anaweza kuangalia mstakabali
wake wa kuhusishwa na tetesi za kwenda Napoli na Paris Saint-Germain ambapo
klabu zote hizo zinakidhi matakwa yake ya kushiriki Ligi ya Mabingwa.