Martina Hingis ambae ni mwanadada nyota wa
tenisi wa zamani, kutoka Switzerland anatarajiwa kurejea
tena katika ulingo wa tenisi baada ya kustaafu mchezo huo mwaka 2007. Hingis
mwenye umri wa miaka 32 amekubali mwaliko wa kucheza michuano ya wazi
ya California ya wawili wawili akiwa sambamba na Daniela Hantuchova
baadae mwezi huu. Nyota
huyo ambaye amewahi kushinda mataji matano ya Grand Slam kwa mchezaji
mmoja mmoja likiwemo taji la Wimbledon mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka
16, Jumamosi iliyopita alichaguliwa kuwa mmoja wa wachezaji mashuhuri
wa mchezo huo kuwahi kutokea. Akihojiwa
kuhusiana na uamuzi huo wa kurejea uwanjani baada ya kupita kipindi
kirefu, Hingis ambaye pia amewahi kushika namba moja katika orodha za
ubora duniani kwa upande wa wanawake amesema bado anahisi kuwa na ari ya
ushindani ndani ya nafsi yake. Mara
ya kwanza Hingis alistaafu mchezo huo akiwa na miaka 22 baada ya
kusumbuliwa na majeraha lakini alirejea tena mwaka 2006 kabla ya
kustaafu tena mwaka 2007 baada ya kukutwa na chembechembe ya dawa za
kusisimua misuli ingawa mwenyewe alikana tuhuma hizo.