Friday, August 15, 2014

SIMBA SC YA DAR YATUA VISIWANI ZANZIBAR KUWEKA KAMBI



Simba sc baada ya kumnasa kocha Mzambia Patrick Phiri na kusaini Mkataba wa mwaka mmoja jana, kikosi cha Simba SC leo kimekwendavisiwani Zanzibar leo kuweka kambi rasmi ya kujiandaa na msimu.

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu na ratiba itatoka wiki moja kabla.

Tayari SImba SC imekamilisha usajili wake na wachezaji wote walikuwa wanahudhuria mazoezi mjini Dar es Salaam.


Phiri amerejea Simba SC baada ya miaka minne tangu aondoke mwaka 2010, akirithi mikoba ya Mcroatia Zdravko Logarusic aliyetupiwa virago mwishoni mwa wiki.

Haijulikani mshahara wa Phiri utakuwa kiasi gani, lakini mara ya mwisho aliondoka Simba SC akiwa analipwa dola za Kimarekani 5,000 (zaidi ya Sh. Milioni 7.5) kwa mwezi. 

Kocha huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2009/2010, aliyezaliwa Mei 3 mwaka 1956, alifanya kazi kwa awamu tatu tofauti akiwa na Wekundu hao wa Msimbazi kati ya mwaka 2004 na 2010 kwa mafanikio makubwa- na sasa anataka kurejesha enzi za wana Simba ‘kutembea vifua wazi’.

Mzambia huyo alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa na Simba SC, misimu ya 2004/2005 na 2009/2010 na pia alishinda Makombe ya Tusker mwaka 2005 la Tanzania na Kenya.