Wednesday, November 19, 2014

KAMATI YA MAREFA TFF YAWAFUNGIA MAREFAWA FDL KESHO NI VPL

KAMATI ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imewaondoa kwenye ratiba za kuchezesha mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) marefa 8 huku ikiwaweka kando makamisaa wawili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) akiwamo Fulgenzi Novatus kutoka Mwanza aliyesimamia mechi ya Kagera Sugar dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Novemba Mosi, mwaka huu.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Saloum Umande Chama ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na makosa mbalimbali yaliyofanywa na marefa na makamisaa hao.
Amesema wumebaini kuna tatizo katika uandikaji wa ripoti za mechi kwa waamuzi na marefa. Pia tumebaini baadhi ya makamisaa wamekuwa wakidai posho kubwa kutoka kwa wasimamizi wa vituo. 
Kamisaa anasafiri kwa nauli ya Sh. 20,000 lakini huku anataka msimamzi amlipe Sh. 30,000 au mara mbili ya nauli halali. Tunaanza kwa kutoa onyo kwao kabla ya kuwashughulikia.
Amesema makamisaa wawili walioondolewa ni pamoja na John Kiteve kutoka Iringa ambaye ameponzwa na taarifa yake kuhusu mechi ya Mbeya City dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya ambayo wenyeji walishinda kwa bao 1-0, bao likifungwa kwa penalti.
Mwingine ni Novatus ambaye taarifa yake kuhusu mechi ya Kagera Sugar dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa wageni kuchapwa bao 1-0 imeonekana kukosa umakini katika kueleza kilichojitokeza uwanjani.
Taarifa ya Kiteve kuhusu mechi ya Mbeya City na Coastal inapishana na maelezo yaliyomo kwenye taarifa ya na refa (Israel Nkongo) pamoja na ofisa wa TFF aliyekwenda kusimamia mchezo huo. 
Mara mpira ulishikwa, mara kuna faulo. Halafu anasema refa alichezesha vibaya lakini mwishoni mwa ripoti anampa alama 8 ambazo ni kiwango kizuri kwa refa wa VPL (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara).
“Fulgence katika ripoti yake anasema mechi ya Yanga na Kagera Sugar iliisha kwa amani na watu walishikana mikono wakati kulitokea fujo na watu kupigana uwanjani.
Amewataja marefa waliofungiwa kuwa ni pamoja na Said Mbege, Hamis Ramadhani na Kalina Kabala (wote kutoka Dar es Salaam). Wengine ni Nassoro Mwinchui, Aloyce Mayombo (wote kutoka Pwani), Thomas Mkombozi (Kilimanjaro), Philimon Mboje (Mwanza) na Mohamed Keyala (Mtwara).

KESHO MAREFA VPL KUWEKWA KITI MOTO.
Aidha, Chama amesema kamati yake kesho itaendelea kupitia mikanda ya mechi zote 49 za raundi saba zilizopita za VPL pamoja na ripoti za marefa, makamisaa na maofisa wa TFF waliotumwa kusimamia mechi hizo.
Malalamiko dhidi ya marefa yamepungua, lakini lengo letu ni kuhakikisha yanaisha. 
aidha kesho tutapitia ripoti na mikanda ya mechi za VPL na waamuzi watakaofanya vizuri tutawapa zawadi, na wale watakaofanya vibaya, tutawapatia wanachostahili pia,” amesema zaidi kiongozi huyo.