Monday, May 27, 2013

BENITEZ ATAKA KUIFUNDISHA TIMU INAYOSHIRIKI LIGI YA MABINGWA ULAYA.

MENEJA wa muda wa klabu ya Chelsea Rafael Benitez ametanabaisha kuwa anataka kufundisha timu inayoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kumaliza kazi yake katika klabu hiyo.
Katika kipindi kifupi kijacho Benitez ataondoka Stamford Bridge akiwa ameisimamia klabu hiyo kwa mara ya mwisho Jumamosi iliyopita wakati walipocheza na Manchester City katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jijini New York Marekani.
Kocha huyo raia wa Hispania ameiongoza Chelsea kushinda taji la Europa League pamoja na kuisadia kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kuajiriwa kwa muda mfupi kuziba nafasi ya Roberto Di Matteo Novemba mwaka jana. 
Banitez anaondoka Chelsea kumpisha Jose Mourinho na kocha huyo sasa anaweza kuangalia mstakabali wake wa kuhusishwa na tetesi za kwenda Napoli na Paris Saint-Germain ambapo klabu zote hizo zinakidhi matakwa yake ya kushiriki Ligi ya Mabingwa.

RADAMEL FALCAO HATIMAYE ATUA KATIKA CLUB YA MONACO

STRAIKA MAHIRI wa Atletico Madrid, Radamel Falcao, atapimwa afya yake kwenye Klabu ya Monaco ambayo imepanda Daraja Msimu huu kurudi Ligue 1 ya France na Uhamisho wake unatarajiwa kugharimu Dau la Pauni Milioni 51.
Habari hizi zimevuja huko Spain na kudaiwa kuwa Atraika huyo kutoka Colombo atapimwa afya yake siku ya Jumatatu Mei 27.
Monaco, ambayo imenunuliwa na Tajiri wa Kirusi Dmitry Rybolovlev, tayari imeshawanunua Mastaa wa FC Porto Joao Moutinho na James Rodriguez kwa Dau la Jumla ya Pauni Milioni 60 na kutua kwa Falcao kutawafanya watatu hao wakutane tena kwani waliwahi kuchezea Klabu moja.
Kuhama kwa Falcao kulidokezwa na Meneja wa Atletico Madrid Diego Simeone ambae ameshasema hatakuwa na kinyongo ikiwa Falcao, mwenye Miaka 27, atahama.
Hivi Juzi, Kocha Msaidizi wa Monaco, Jean Petit, alidokeza wanatarajia Falcao na Wachezaji wengine wanne au watano wa kiwango chake kununuliwa na Klabu yao.
Mwezi Desemba 2011, Dmitry Rybolovlev alinunua Hisa za Asilimia 60 za Klabu ya Monaco na kuanza kuibadili wakati huo ikiogelea Daraja la chini huko France, Ligue 2, na Mwezi Mei 2012 alimteua Kocha wa zamani wa Chelsea Claudio Ranieri kuiongoza Monaco na amefanya hilo kwa mafanikio kwa kuirudisha Monaco Daraja la juu huko France.

NEYMAR HATIMAYE SASA ATUA FC BARCELONA

CLUB ya soka FC Barcelona imefikia Makubaliano na Klabu ya Brazil, Santos, ya kumsaini Neymar ambapo leo Jumatatu Mei 27 atasaini Mkataba ili kukamilisha Dili hiyo ya Uhamisho.
Klabu ya Barcelona imetoa Taarifa rasmi ya kuthibitisha kufikia makubaliano ya kumsaini Nyota huyo wa Brazil mwenye Miaka 21.
WASIFU:
Neymar da Silva Santos Junior
KUZALIWA: 5 Februari 1992, Nchini Brazil
Santos: Mechi 229 Magoli 138
Brazil: Mechi 32 Magoli 20
Na Mwenyewe Neymar alitoa Ujumbe kwenye Mtandao wa Instagram uliosema  kuwa jumatatu nasaini Mkataba na Barcelona. Nataka kuwashukuru Mashabiki wa Santos kwa Miaka hii 9 ya ajabu.
Juzi Klabu ya Santos ilitoa Taarifa kuwa imepokea Ofa mbili za kumnunua Neymar na ilisadikiwa zimetoka toka mbili kati ya Klabu za Barcelona, Real Madrid au Chelsea.
Mkataba wake na Santos ulitarajiwa kumalizika mwishoni mwa Msimu ujao, Mwezi Juni 2014.
Neymar anatarajiwa kujiunga na Barcelona mara baada ya kuiwakilisha Brazil kwenye Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara yatakayochezwa Nchini Brazil kuanzia Juni 15 hadi 30.
Neymar ndie ameiongoza Santos kupata mafanikio makubwa tangu Nguli Pele aache kuichezea Klabu hiyo kwenye Miaka ya 1970 kwa kuisaidia kutwaa Kombe la Brazil Mwaka 2010, Copa Libertadores Mwaka 2011 na Ubingwa wa Jimbo la Sao Paolo kwa mara 3 mfululizo.
Nayo Klabu ya Santos imesema kuwa ilijaribu kila njia ili Neymar abaki kwao lakini Ofa za nje zimewafanya wasiweze kushindana.
Hata hivyo, Santos imekataa kutaja Dili hiyo ya Uhamisho imegharimu kiasi gani kwa vile kila upande umekubaliana kuwa iwe siri.
             
WASIFU WA NEYMAR
Taarifa kuhusu yeye
Full name Neymar da Silva Santos Júnior
Date of birth 5 February 1992 (age 21)
Place of birth Mogi das Cruzes, Brazi
Height 1.74 m (5 ft 9 in)
Playing position Mshambuliaji
Club ya sasa
Current club Santos
Number 11
Timu za ujana
1999–2003 Portuguesa Santista
2003–2009 Santos
Timu ya ukubwa
Years Team Mechi Goli
2009– Santos 103 (54)
Timu ya Taifa
2009 Brazil U17 3 (1)
2011 Brazil U20 7 (9)
2012 Brazil U23 7 (4)
2010– Brazil 32 (20)

AGUERO BADO NIPO NIPO MAN CITY MPAKA 2017.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Manchester City, Sergio Aguero ameongeza mkataba wa mwaka mmoja ambao utamuweka katika klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uingereza mpaka mwaka 2017. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 24 amefunga mabao 12 katika mechi 30 za ligi alizocheza msimu uliopita na kufunga bao la ushindi dhidi ya Queens Park Rangers lililowapa taji la ligi katika msimu wa 2011-2012. Mara baada ya kusaini mkataba huyo Aguero aliuambia mtandao wa klabu hiyo kwamba anajisikia furaha na kuhitajika hivyo atafanya kila awezalo ili aendelee kufanya kazi vyema na kuipa mataji klabu hiyo. Vyombo vya habari nchini Uingereza vilikuwa vikiripoti kuwa mchezaji huyo anaweza kutimkia Real Madrid lakini tetesi hizo zitakwisha baada ya kuwa mchezaji mwingine wa timu hiyo kuongeza mkataba baada ya Gael Clichy, Yaya Toure na David Silva kufanya hivyo.

KLOPP ASEMA TUTAIMARISHA KIKOSI FAINALI ZIJAZO

MENEJA wa klabu ya Borussia Dortmund, Jurgen Klopp ametanabaisha kuwa ataimarisha kikosi chake na kufikia fainali nyingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kipigo walichopata dhidi ya Bayern Munich. Dortmund walipoteza mchezo huo ulizikutanisha timu zote kutoka Ujerumani kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Wembley baada ya bao la dakika za mwisho lililofungw ana Arjen Robben. Lakini kocha huyo ametamba kuwa pamoja na kushindwa katika fainali hiyo ya Wembley lakini anaamini atafikia fainali nyingine katika kipindi kifupi kijacho. Klopp amesema kwasasa ana kazi kubwa ya kuimarisha kikosi chake baada ya wachezaji kadhaa tegemeo kutaka kuondoka mwishoni mwa msimu huu lakini anaamini mpaka kufikia msimu mpya tayari atakuwa na kikosi imara. Kiungo tegemeo wa klabu hiyo Mario Gotze tayari imeshathibitishwa kwenda Bayern Msimu ujao huku mshambuliaji wake nyota Robert Lewandowski naye akijipanga kuelekea huko.

TAIFA STARS YAELEKEA ADDIS ABABA LEO.

TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajia kuondoka leo (Mei 26 mwaka huu) usiku kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambapo itaweka kambi na kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya kwenda Morocco. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka saa 5 usiku kwa ndege ya EgyptAir ikiwa na kikosi cha wachezaji 21 chini ya nahodha wake kipa Juma Kaseja. Timu hiyo ikiwa Ethiopia, Juni 2 mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan ambapo siku inayofuata itaondoka kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri. Mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itachezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.

Mbali ya nahodha Kaseja, wachezaji wengine wanaoondoka katika kikosi hicho ambacho kina wiki sasa tangu kingie kambini jijini Dar es Salaam ni Mwadini Ally na Ally Mustafa ambao wote ni makipa. Wengine ni Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Aggrey Morris, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo. Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wako na timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watajiunga moja kwa moja na Stars jijini Marrakech, Juni 4 mwaka huu wakitokea Maputo, Msumbiji mara baada ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Liga Muculumana ya huko. Katika msafara huo wa Ethiopia benchi la ufundi la Stars linaundwa na Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi),Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja wa timu), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).

Saturday, May 25, 2013

30 TWIGA STARS WAITWA KAMBINI KESHO MEI 26 MWAKA HUU

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu (Twiga Stars), Rogasian Kaijage amewaita kambini wachezaji 30 ikiwa ni mwendelezo wa kuijenga na kuiimarisha timu hiyo.

Twiga Stars itakuwa na kambi ya siku kumi kuanzia Jumapili (Mei 26 mwaka huu) ambapo baadaye inatarajia kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya wachezaji kurudi kwenye klabu zao.

Kambi hiyo ni mwendelezo wa programu iliyopendekezwa na kocha kuijenga na kuiimarisha timu hiyo kwa vile haina mashindano mwaka huu, na itakuwa kambi ya pili baada ya ile iliyofanyika Machi mwaka huu.

Wachezaji walioitwa na klabu zao kwenye mabano ni Asha Rashid (Mburahati Queens), Aziza Mwadini (Zanzibar), Belina Julius (Lord Barden), Ester Chabruma (Sayari), Ester Mayala (TSC Academy), Eto Mlenzi (JKT), Evelyn Sekikubo (Mburahati Queens) na Fatuma Bushiri (Mburahati Queens).

Fatuma Hassan (Mburahati Queens), Fatuma Omari (Sayari), Flora Kayanda (Tanzanite), Hamisa Athuman (Marsh Academy), Hellen Peter (JKT), Maimuna Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Tanzanite), Mwanahamisi Omari (Mburahati Queens), Mwanaidi Tamba (Mburahati Queens) na Mwapewa Mtumwa (Sayari).

Nabila Ahmed (Marsh Academy), Pulkeria Charaji (Sayari), Rehema Abdul (Lord Barden), Rukia Khamis (Uzuri Queens), Semeni Abeid (Tanzanite), Sharida Boniface (Makongo Sekondari), Sophia Mwasikili (Sayari), Therese Yona (TSC Academy), Vumilia Maarifa (Evergreen) na Zena Khamis (Mburahati Queens).

RCL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI KESHO
Raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inaendelea kesho (Mei 26 mwaka huu) kwa mechi sita za kwanza zitakazochezwa katika miji sita tofauti.


Abajalo ya Dar es Salaam na Kariakoo ya Lindi zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam wakati Machava FC ya Kilimanjaro itakuwa mwenyeji wa Mpwapwa Stars ya Dodoma kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Nayo Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida huku Polisi Jamii ya Bunda mkoani Mara ikimenyana na Biharamulo FC ya Kagera kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Mjini Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika ni kati ya wenyeji Saigon FC na Katavi Warriors ya Katavi wakati Njombe Mji itaikaribisha Kimondo SC ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

Leo (Mei 25 mwaka huu) Friends Rangers ya Kinondoni, Dar es Salaam inacheza na African Sports ya Tanga kwenye Uwanja wa Azam Chamazi. Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.

Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)