Tuesday, June 11, 2013

MOURINHO KWA MARA NYINGINE ATAMBULISHWA RASMI DARAJANI.

Kocha jose mourinho rasmi  ametambulishwa darajani ambapo amesisitiza  na kuweka wazi kuwa hajawahi kuwa na bifu na mmiliki wa club hiyo Roman Abramovich na lengo lake kuu ni kumrejesha John Terry uwanjani huku akiwataka wachezaji kucheza kwa uzalendo mkubwa.
mourinho2 7c61aMreno Jose Mourinho jana ametambulishwa rasmi kuwa kocha mpya wa wazee wa darajani, klabu ya Chelsea. 
Akizungumza na waandishi wa habari, Mourinho ambaye miaka ya nyuma akiwa na Chelsea alikuwa anajiita “The Speacial one” kwa tafsiri isiyo rasmi,  akimaanisha mtu maalumu, leo hii ametoa kali ya mwaka baada ya kubadili jina hilo na kujiita “The Happy One kwa tafsiri isiyo rasmi unaweza kusema “Mtu mwenye furaha pekee”.
Mreno huyo ambaye ametokea klabu ya Real Madridi ya Hispania leo mchana ametambulishwa jijini London na kujibu maswali mengi kutoka kwa wanahabari waliohitaji kujua mambo mengi kutoka kwake likiwemo suala la uhusiano na bosi wake Abramovich.
Mourinho ambaye miaka ya nyuma alitimuliwa na mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich baada ya kushindwa kuelewana, leo hii amesema kipindi cha nyuma alikuwa na mahusiano mazuri na bosi wake, endapo wangekuwa na mahusiano mabaya asingerejea kwa mara ya pili darajani.
Akiongea na wanahabari wapatao 250 leo katika uwanja wa Stamford Bridge, aliulizwa kama ataendelea kujiita “The Special one”, kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 kwa sasa alisema “I am the Happy One” na kumalizia maneno yake kwa kusema “nina furaha sana”.
mourinho3 f5edf
Mourinho alisema ” Mambo mengi sana yametokea katika maisha yangu ya kufundisha soka na kazi yangu miaka tisa iliyopita, lakini ni mtu yule yule, nina moyo uleule, nina hisia zile zile za kupenda mpira na kazi yangu, lakini kwa sasa ni mtu mwingine kabisa baada ya kurudi nyumbani Chelsea, nina furaha sana”.

Mourinho amewataka wachezaji wake kujituma zaidi na kuongeza kuwa klabu ni muhimu kuliko wao, kwani isingekuwepo wao pia wasingekuwepo. Chanzo: Baraka Mpenja

SNEIJDER ASIKITISHWA KUNYANG'ANYWA UNAHODHA:

KIUNGO nyota wa klabu ya Galatasaray  na timu ya taifa ya Uholanzi Wesley Sneijder amekiri kusikitishwa na kitendo cha kunyang’anywa kitambaa cha unahodha wa timu yake ya taifa. Kiungo huyo alipewa unahodha wa Uholanzi wakati Louis van Gaal alipochukua nafasi ya Bert van Marwijk baada ya michuano ya Ulaya 2012. Akihojiwa Sneijder amesema ni jambo lililomuumiza sana na sio sababu hakutambua hilo ila kwasababu amekua akijitoa kwa uwezo wake wote toka akabidhiwe majukumu hayo lakini inabidi akubaliane na uamuzi wa kocha. Baada ya kumvua unahodha kiungo huyo kutokana na kutofurahishwa na kiwango chake, Van Gaal alimkabidhi majukumu hayo mshambuliaji nyota wa Manchester United Robin van Persie ambaye ameisadia klabu yake kushinda taji la Ligi Kuu msimu uliopita.

ZINEDINE ZIDANE AWEKA WAZI KUWA WATAKA KUVUNJA REKODI YA USAJILI.

Mkurugenzi wa michezo wa klabu ya REAL MADRID ambaye alikuwa kiungo wa wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Real Madrid, Zinedine Zidane amekiri kuwa lengo kuu ni kuvunja rekodi ya uhamisho kama watkuwa na nia ya kumsajili Gareth Bale. 
Bale ambaye ni winga wa klabu ya Tottenham Hotspurs ya Uingereza amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Madrid ambapo kuna taarifa kuwa klabu hiyo imetenga kitita cha paundi milioni 85 kwa ajili yake.
Kama uhamisho huo ukifanyika utakuwa umevunja rekodi aliyoweka Cristiano Ronaldo wakati aliposajiliwa kutoka Manchester United kwa ada ya paundi milioni 80 miaka minne iliyopita. 
Zidane amesema kwa kiwango cha mchezaji huyo alichokionyesha msimu uliopita sio ajabu vilabu vingi kumuwania ndio maana anadhani itakuwa gharama kubwa kupata saini yake. 
Nyota huyo wa zamani aliendelea kusema kuwa kama klabu yoyote yenye uwezo wa kifedha itahitaji saini ya mchezaji huyo lazima watoe dau kubwa na hata kufikia kuvunja rekodi ili Tottenham waweze kumuachia.

Monday, June 10, 2013

PEREIRA RASMI KUIFUNDISHA AL AHLI YA SAUDI ARABIA.

KLABU ya Al Ahli ya Saudi Arabia imethibitisha na kuweka wazi kuwa imemteua Vitor Pereira kuwa kocha mpya wa klabu hiyo baada kocha huyo kuondoka Porto mwishoni mwa msimu huu. Pereira ameifundisha Porto kwa kipindi cha misimu miwili baada ya kuchukua nafasi ya Andre Villas-Boas Juni mwaka 2011 na kuisadia klabu hiyo kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu nchini Ureno. Katika taarifa iliyotolewa katika mtandao wa klabu hiyo, Pereira mwenye umri wa miaka 44 atajiunga rasmi na klabu hiyo Juni 27 kabla ya kuiandaa timu kwa ajili ya msimu ujao siku mbili baadae. Pia zimekuwepo taarifa kuwa atatua katika klabu hiyo na wasaidizi wake wa watatu kutoka Ureno kwa ajili ya kuimarisha benchi lake la ufundi.

MMOJA APOTEZA MAISHA KATIKAMICHUANO YA LANGALANGA YA CANADIAN.

MASHINDANO ya langalanga ya Canadian Grand Prix jana yalimalizika kwa Majonzi makubwa baada ya mmoja wa wafanyakazi mwenye umri wa miaka 38 kufariki baada ya kukanyagwa na winji. Ajali hiyo ilitokea wakati gari la dereva Esteban Gutierrez wa timu ya Sauber lilipokuwa likiondolewa barabara za Montreal baada ya kupata ajali.

Mashuhuda wanasema wakati winji hilo likijaribu kuliondoa gari hilo ndipo mfanyakazi huyo aliangusha radio yake na wakati akiiokota ndipo alipokanyagwa kwasababu dereva wa winji hakumuona. Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter Gutierrez alituma salamu zake za rambirambi kwa familia ya mfanyakazi huyo kwa kumpoteza mtu wao karibu. Mbali na Gutierrez madereva wengine waliotoa rambirambi zao ni pamoja na Sebastian Vettel wa Red Bull aliyeshinda mbio hizo pamoja na Fernando Alonso wa Ferrari aliyeshika nafasi ya pili. Hilo ni tukio la pili kutokea katika mashindano hayo kwani mwaka jana katika michuano ya Grand Prix ya Italia mfanyakazi wa kujitolea wa zimamoto Paolo Ghislimberti alifariki kutoka na amejraha aliyopata kichwani na kifuani baada ya kupigwa na tairi lililochomoka kutoka katika gari la Heinz-Harald Frentzen wa timu ya Jordan.

TAIFA STAR YATUA NCHINI IKITOKEA NCHINI MORROCO.

TIMU ya taifa ya  Tanzania, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imewasili  nchini leo asubuhi.
Taifa stars ilikuwa Morocco kucheza na wenyeji wao ambapo katika mchezo huo taifa star imefungwa bao 2-1 katika mechi ya Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.

Stars ambayo bado inashika nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi sita imewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Aidha katika kundi c kinara wa kundi hilo ni Ivory Coast yenye point kumi ambayo itacheza mchezo wa marudiano na Taifa Star wikiendi ijayo katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Hata hivyo kwa upande wa kundi hilo nafasi ya tatu inashikiliwa na Morocco yenye point tano huku nafasi ya mwisho ikishiliwa na Gambia yenye point moja.
KUNDI C


Pos
Team
P
W
D
L
GF
GA
GD
Pts
1
Ivory Coast
4
3
1
0
10
2
8
10
2
Tanzania
4
2
0
2
6
6
0
6
3
Morocco
4
1
2
1
6
7
-1
5
4
Gambia
4
0
1
3
2
9
-7
1

Friday, June 7, 2013

TAIFA STARS SASA INAJITOSHELEZA- TENGA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeishukuru Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kuiwezesha timu ya taifa, Taifa Stars kuondokana na matatizo na kuwaomba Watanzania kuiombea timu ili ifanye vizuri katika mechi yake ya kesho (Juni 8 mwaka huu) dhidi ya Morocco mjini Marrakech.
Stars, ambayo inashika nafasi ya pili kwenye kundi lake la mashindano ya awali ya Kombe la Dunia ikiwa nyuma ya Ivory Coast kwa tofauti ya pointi moja, inacheza na Morocco katika mechi ya nne itakayofanyika Marrakech baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Dar es Salaam mwezi Machi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema kuwa tangu kuanza kwa udhamini, TFF haijawahi kupata udhamini mkubwa kama wa Kilimanjaro Premium Lager ambayo imeingia mkataba wa miaka mitano wa kuidhamini Stars wenye thamani ya dola milioni 10 za Marekani.

“Katika kipindi chote hiki hatujawahi kupata udhamini ambao umekidhi mahitaji yote ya timu kama huu wa TBL,” alisema Tenga kwenye mkutano na waandishi uliofanyika kwenye ofisi za TFF.

“Lakini katika mwaka mmoja uliopita (tangu TBL ianze kudhamini) hatujawahi kushindwa kuisafirisha timu; kushindwa kulipa posho za wachezaji; kutanguliza watu wetu kwenda nje kuiandalia timu sehemu nzuri; kuzilipia tiketi za ndege timu tunazocheza nazo mechi za kirafiki na hata kuzilipia ada ya kucheza mechi (appearance fee).

“Posho za wachezaji zimepanda kwa karibu mara mbili na ndio maana leo wachezaji wanaijali timu yao. Yote haya ni kutokana na udhamini huu. Watu wanasema usione vinaelea….”

Tenga alisema kuwa udhamini huo ndio sasa umeanza kuzaa matunda na timu inafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na maandalizi ya muda mrefu.

“Sasa tunawaomba Watanzania waiombee timu na tunawashukuru wale waliokwenda Morocco kuishangilia kwa kuwa vijana wetu wanapata nguvu pale wanapoona kuna watu wako nyuma yao,” alisema Tenga.

Rais huyo wa TFF pia alisifu kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuiita timu Ikulu na kuongea na kula na wachezaji, akisema kitendo hicho kitasaidia kuongeza hamasa kwenye timu.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema kampuni yake itaendelea kuwa bega kwa bega na TFF na kwamba uhusiano baina ya pande hizo mbili umeimarika na utaendelea kuimarika.

Katika mkutano huo, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilikabidhi fulana maalum kwa ajili ya mashabiki ambao wamekwenda Morocco kuishangilia timu.

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu alisema tayari fulana 250 zimegawiwa kwa mashabiki walioko Morocco na nyingine zilitarajiwa kusafirishwa jana.

USHIRIKI DARFUR MIKONONI MWA SERIKALI- TENGA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.

Tenga, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF, alisema tayari TFF na Serikali zimeshafanya mazungumzo, na Serikali imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa Serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya kutoa tamko.

“Masuala ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.

“Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.
“Kama tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.”

Tenga alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo.

Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama.

“Hivyo nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali,” alisema Tenga.

“Lakini napenda kuishukuru Serikali ya Sudan kwa uamuzi huo kwa sababu kuandaa mashindano hayo si kitu kidogo. Tayari Katibu Mkuu wa CECAFA (Nicholas Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo hayo na kukaa wiki nzima akikagua viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika nazo,” alisema.

Alisema watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu Darfur.

“Mhe. Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni nzuri… alisema Serikali haitakubali kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,” alisema Tenga.

“Kwa maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali taarifa zote muhimu kuhusu hali itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa tunasubiri tamko la Serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza tupata uhakika wa usalama kutoka serikalini ndipo tuziite timu.”

Alifafanua kuwa si jukumu la CECAFA kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama cha nchi mwenyeji ndicho kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.

“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo hayo mawili ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao mashindano hayo yafanyike kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia CECAFA usalama,” alisema.



“Sasa ikitokea Serikali yetu ikasema hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende kwa sababu masuala ya usalama yako nje ya CECAFA.”

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)