Wednesday, July 10, 2013

DOS SANTOS AKAMILISHA USAJILI KATIKA CLUB YA VILLAREAL"

Kiungo nyota wa kimataifa wa Mexico, Giovani Dos Santos amekamilisha usajili wake wa kujiunga na klabu Villareal ambayo imepanda ligi msimu huu akitokea klabu ya Real Mallorca zote za Hispania. Dos Santos mwenye umri wa miaka 24 ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Mexico kilichonyakuwa medali ya dhahabu katika michuano ya olimpiki jijini London mwaka jana, amesaini mkataba wa miaka minne na klabu hiyo. Kiungo huyo mshabuliaji aliibukia katika shule ya watoto ya Barcelona kabla ya kwenda katika klabu ya Tottenham Hotspurs mwaka 2008 kwa uhamisho wa euro milioni sita. Hata hivyo Dos Santos alishindwa kung’aa sana katika kikosi cha kwanza na kujikuta akipelekwa kwa mkopo katika timu ya daraja la pili ya Ipswich Town na baadae kwenda Galatasaray ya Uturuki na Racing Santander.

WANNE KUTOKA BAYEN MUNICH NAO KATIKA ORODHA YA FIFA

Club ya Bayern Munich ya ujerumani imefanikiwa kutoa wachezaji wa nne walioteuliwa katika orodha ya wachezaji 10 na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA kugombea tuzo ya mchezaji bora wa bara hilo kwa msimu wa 2012-2013. Wachezaji hao ni Franck Ribery, Thomas Mueller, Arjen Robben na Bastian Schwainsteiger ambao wote walikuwemo katika kikosi cha Bayern ambacho kilifanikiwa kunyakuwa mataji matatu msimu uliopita. Mbali na hao wengine waliotajwa katika orodha hiyo ni mchezaji bora wa mwaka katika Ligi Kuu nchini Uingereza, Gareth Bale pamoja na mfungaji bora wa ligi hiyo Robin van Persie huku Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakiwa wachezaji pekee kutoka La Liga ya nchini Hispania kwenye orodha hiyo. Hii itakuwa ni mara ya tatu kufanyika sherehe za tuzo hizo ambapo mwaka 2011 Messi ndiye aliyeshinda huku mchezaji mwenzake wa Barcelona Andres Iniesta akishinda tuzo hiyo mwaka jana. Wachezaji wengine ni Mshambuliaji nyota wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG, Zlatan Ibrahimovic na Robert Lewandowski anayekipiga Borussia Dortmund ambapo orodha ya mwisho ya wachezaji watatu itatajwa Agosti 6 kabla ya sherehe za kumjua mshindi ambazo zitafanyika wakati wa upangaji wa ratiba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Agosti 29 mwaka huu jijini Monaco.

Tuesday, July 9, 2013

MURRAY APONGEZWA NA CAMEROON VS MALIKIA ELIZABETH


Waziri Mkuu David Cameron pamoja na Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza wamekuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliotoa pongezi kwa mchezaji tenisi nyota wan chi hiyo Andy Murray kwa kunyakuwa taji la michuano ya Wimbledon. Wachezaji nyota na watu wengine maarufu nchini humo pia walitoa pongezi zao kwa Murray mwenye umri wa miaka 26 baada ya kuwa Muingereza wa kwanza kunyakuw ataji la michuano hiyo toka Fred Perry alipofanya hivyo mwaka 1936, kwa kumfunga Novak Djokovic kwa seti 3-0. 
Cameron ambaye alikuwepo uwanjani kushuhudia mtanange huo alimpongeza Murray kwa kuonyesha kiwango cha juu kwenye mchezo huo na kuweka historia mpya katika mchezo huo nchini Uingereza. Mwandishi wa BBC katika kasri ya kifalme nchini humo, Peter Hunt alibainisha kuwa Malkia alimtumia ujumbe binafsi Murray kumpongeza kwa kufanikiwa kushinda taji hilo.

LIVERPOOL YAIBWAGA CHINI OFA YA ARSENAL KUHUSU SUAREZ

Majogoo wa jiji london Club ya soka ya Liverpool imepiga chini ofa ya paundi milioni 30 waliyotoa Arsenal kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo Luis Suarez. Kumekuwa na tetesi za muda mrefu za Suarez kutaka kuuzwa baada ya kufungiwa mechi 10 kwa kumng’ata beki wa Chelsea Branislav Ivanovic katika Uwanja wa Anfield msimu uliopita. Klabu ya Real Madrid ya Hispania ndio wanaotegemewa kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay baada ya kutamka wazi kwamba ameyachoka maisha ya Uingereza. Mwishoni mwa wiki hii Arsenal nao walidaiwa kuingia katika kinyang’anyiro cha kumuwania lakini Liverpool walikataa kutoa kauli yoyote kuhusiana na tetesi hizo huku wakisisitiza kwamba bado wanamhitaji mshambuliaji huyo.

THIERRY HENRY NAYE YUMO KIKOSI CHA WACHEZAJI 10 WA MLS

Mshambuliaji nyota wa zamani wa Ufaransa, Thierry Henry ni moja kati ya wanadinga nyota 10 watakaounda kikosi kutoka katika Ligi Kuu ya Soka nchini Marekani-MLS ambacho kitapambana na AS Roma ya Italia Julai 31 huko jijini Kansas. Henry mwenye umri wa miaka 35 mshambuliaji wa klabu ya New York Red Bull ambaye aliisadia Ufaransa kushinda Kombe la Dunia mwaka 1998, amefunga mabao sita katika mechi 17 alizoichezea timu hiyo msimu huu. Kabla ya kwenda Marekani mwaka 2010 akitokea klabu ya Barcelona, henry amewahi kucheza katika vilabu vya Juventus na Arsenal. Golikipa wa FC Dallas ambaye ni raia wa Peru Raul Fernandez, kiungo wa timu ya taifa ya Canada Will Johnson na Beki wa Kansas City Aurelien Collin ambaye ni raia wa Ufaransa ni miongoni mwa wachezaji wasiokuwa raia wa Marekani walioteuliwa katika kikosi hicho cha nyota wa MLS.

FIFA-SEPP BRATTER ATARAJI KUZUNGUMZA NA MAOFISA WA ISRAEL

Bratter akiyatafakari mazungumzo
Sepp Blatter rais wa Shirikisho la Soka Dunia-FIFA amemweleza kiongozi wa michezo nchini Palestina kuwa atazungumza na maofisa wa Israel ili kujaribu kuondoa vizuizi vya kusafiri walivyowekewa wachezaji wa taifa hilo. Blatter alitarajiwa kukutana na ofisa mkuu wa soka nchini Israel kabla ya kuzungumza na kiongozi wa kisiasa wan chi hiyo waziri mkuu Benjamin Netanyahu kuzungumzia suala hilo. Palestina wamekuwa wakichukizwa na vikosi vya usalama vya Israel ambavyo vinalinda mji wa Gaza kuwazuia wanamichezo wa taifa hilo kusafiri kwa uhuru katika pande hizo mbili. Blatter amesema atakwenda Israel sio kwenda kukitetea Chama cha Soka cha Palestina lakini pia kutetea misingi ya kanuni za FIFA ambayo ni kuunganisha watu na sio kuwagawa.

MESSI RASMI ATARAJIWA KUREJEA BARCA MAZOEZINI JULAI 15

Mshambuliaji nyota wa kimataifa wa argentina na club ya fc Barcelona, Lionel Messi anatarajiwa kurejea mazoezini Julai 15 baada ya kupumzika kwa wiki moja pekee katika likizo yake kutokana na majukumu mbalimbali ambayo yamekuwa yakimtinga. Masimu wa 2012-2013 kwa mchezaji huyo nyota ulimalizika Juni 15 baada ya Argentina kuigaragaza Guatemala kwa mabao 4-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki, hivyo kumanisha kwamba nyota huyo angekuwa na mwezi mzima wa kupumzika kabla ya kuanza kwa msimu mpya. Hata hivyo Messi mwenye umri wa miaka 26 alitumia nafasi hiyo kucheza mechi mbalimbali za hisani kuzunguka dunia na kumaliza ziara yake hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita huko Chicago, Marekani. Jumla ya ziara zote hizo Messi amesafiri kilimita zaidi ya 90,000 toka msimu wa ligi ulipomalizika akitembelea nchi za Argentina, Ecuador, Guatemala, Italia, Senegal, Colombia, Peru na Marekani. Nyota huyo amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya msuli mwishoni mwa msimu uliopita na mapumziko mafupi aatakayopata yatawapa uhakika mdogo madaktari juu ya afya yake kabla ya kuanza msimu mpya wa 2013-2014.