Tuesday, July 16, 2013

FIFA BADO USO KWA USO NA CAMEROON KATIKA MICHEZO

Shirikisho la Soka Duniani-FIFA limedai kuwa klabu ya Coton Sport ya Cameroon haitaruhusiwa kucheza mechi yao ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika mwishoni mwa wiki hii kwasababu ya adhabu iliyopewa Shirikisho la Soka la nchi hiyo-Fecafoot na FIFA. Hatua ya kuzuiwa kwa klabu hiyo kunazidi kuleta utata katika michuano hiyo mikubwa kabisa ya vilabu barani Afrika huku mahasimu wa soka nchini Misri klabu ya Zamalek na Al Ahly ambao ndio mabingwa watetezi nao wakiwa hawajui hatma ya mechi baina yao kwasababu ya vrugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo. Timu nane zilizofanikiwa kuvuka hatua ya makundi, ndio zinatarajiwa kuchuana kutafuta washindi watakaocheza nusu fainali ya michuano hiyo katika mechi zao za kwanza mwishoni mwa wiki hii. FIFA imesema kuwa tayari wameshaanza mazungumzo kujaribu kutatua mgogoro wa Cameroon lakini mpaka sasa hakuna lolote lililofikiwa mpaka kuwashawishi kuondoa adhabu ya kuifungia nchi hiyo kushiriki michuano yoyote ya kimataifa waliyoitoa Julai 4 mwaka huu. Kufungiwa kwa Cameroon kumekuja kufuatia uchaguzi wa Juni 19 ambao Mohammed Iya alichaguliwa tena kuongoza Fecafoot pamoja na kukamatwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha wakati akiongoza kampuni ya Cotton Development Corporation inayomiliki timu ya Cotton Sport.

REAL MADRID YATAJWA KUWA CLUB YENYE THAMANI ZAIDI DUNIANI

CLUB ya Real Madrid ya Hispania imetajwa kuwa klabu yenye thamani zaidi katika orodha ya timu za michezo 50 zenye thamani zaidi duniani iliyotolewa na jarida Forbes la nchini Marekani. Katika orodha hizo timu za Ligi Kuu ya Mpira wa Kimarekani-NFL ndizo zilizoonekana kutawala kwa kiasi kikubwa. Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na jarida hilo Madrid ambao ni mabingwa mara tisa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wana utajiri unaofikia dola bilioni 3.3, utajiri huo ukiwa umeongezeka kwa dola bilioni 1.88 kulinganisha na mwaka uliopita baada ya kuongeza mapato yao kwa kuingia mikataba na kampuni za Adidas na Shirika la Ndege la Emirates. Manchester United wamepigwa kikumbo na Madrid na kushuka mpaka nafasi ya pili wakiwa na utajiri wa dola bilioni 3.17 wakati mabingwa wa Hispania Barcelona wao wamekwea kutoka nafasi ya tano mpaka ya tatu wakiwa na utajiri unaofikia dola bilioni 2.6. Nafasi ya nne inashikiliwa na timu ya Baseball ya Marekani ya New York Yankees ambao wana dola bilioni 2.3, wakifuatiwa na Dallas Cowboys ya NFL dola bilioni 2.1 na New England Patriots dola bilioni 1.6. Nyingine ni Los Angeles Dodgers ya baseball dola bilioni 1.6, timu za NFL Washington Redskins na New York Giant pamoja na klabu ya soka ya Arsenal ya Uingereza ambazo zote hizo zina utajiri wa dola bilioni 1.3.

KAMPUNI YA VIFAA VYA MICHEZO ADIDAS YA SIMAMISHA MKATABA WA TYSON GAY

Kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas imesimamisha mkataba wake wa udhamini na mwanariadha nyota wa mbio fupi Tyson Gay wa Marekani baada ya kukutwa na chembechembe za dawa za kuongeza nguvu. Msemaji wa kampuni alidai kuwa awameshtushwa na tuhuma hizo kwa Gay na hata kama bado hajakutwa na hatia ya kosa hilo moja kwa moja kampuni itasimamisha udhamini wake mpaka hapo hukumu itakapotolewa. Gay mwenye umri wa miaka 30, ndio mwanariadha wa pili mwenye kasi zaidi duniani katika mbio za mita 100 akiwa sambamba na Yohan Blake wa Jamaica na pia ndiye mwanariadha aliyeweka rekodi ya kasi zaidi kwa mwaka huu. Nyota huyo ambaye aliwahi kuwa bingwa wa dunia katika mbio za mita 100, 200 na mita 400 kupokezana vijiti mwaka 2007 alishindwa kukata tuhuma hizo na kudai kuwa alimwamini mtu ambaye alimwangusha na hivyo atapokea adhabu yoyote atakayopewa.

Sunday, July 14, 2013

Coastal Union yanasa saini ya Udula wa Bandari ya Kenya


Na Paul Mkai,Tanga.
UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga umesema tayari umeshamalizana na aliyekuwa mshambulizi wa timu ya Bandari ya Kenya,Christian Udula kwa mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuichezea timu kwenye msimu mpya ambao utaanza Agosti mwaka huu.

Akizungumza na Blogg hii,Katibu Mkuu wa timu ya Coastal Union ya Tanga,Kassim El Siagi alisema baada ya kumalizina na mchezaji huyo anatarajiwa kutua mkoani Tanga wiki ya leo akiwa na mchezaji mwengine wa timu hiyo Jerry Santos.

Siagi alisema msimu huu wamedhamiri kufanya usajili wa nguvu ambao utaifanya timu hiyo kuwa tishio kwenye mechi zao za Ligi kuu ya Tanzania bara kwani malengo yao ni kuchukua ubingwa wa mashindano hayo makubwa hapa nchini.

Aidha alisema timu hiyo itacheza mechi mbalimbali za majaribio nchini Kenya na timu za Sofapaka,Bandari na Goromahia lengo likiwa ni kukipa makali kikosi hicho ambacho kinatarajiwa kuwa tishio.

Katibu huyo aliwataka wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kuendelea kujitokeza kuisapoti timu hiyo ili iweze kutimiza azma yao waliyojiwekea kwenye michuano hiyo.

Mwisho.

Friday, July 12, 2013

KAMPUNI YA MADUKA NCHINI BRAZIL WATISHIA KWENDA MAHAKANI KUHUSU USAJILI NEYMAR

Kampuni ya DIS inayomiliki maduka makubwa nchini Brazil na ambao wanamiliki asilimia 40 ya haki za usajili wa Neymar wametishia kwenda mahakamani kuhusiana na mgao wao kwa nyota huyaa o katika usajili wake kwenda Barcelona. Kampuni hiyo inayoendeshwa na Idi Sonda imedai kuwa na haki ya kupata fedha zaidi juu ya makubaliano ya ziada kati ya klabu ya Santos na Barcelona ambayo yako nje ya ada ya uhamisho wake ambayo ilifikia kiasi cha euro milioni 57. Mkurugenzi Mtendaji wa DIS, Roberto Moreno ameomba kupewa taarifa kamili ya hati ya uhamisho wa Neymar kwenda Barcelona ili kupata ufafanuzi kuhusu malipo ya baadae watakayopewa Santos. Moreno amesema mpaka kipindi hicho hawajaonyeshwa hati yoyote, hivyo atafunga safari kwenda makao makuu ya Santos kufuatilia hati hiyo na baada ya hapo wataamua kama watahitaji kwenda mahamani. Hatua ya kampuni hiyo imekuja kufuatia taarifa zilitolewa na vyombo vya habari nchini humo kwamba Santos watapata nyongeza ya euro milioni mbili kama mchezaji huyo atakuwemo katika orodha ya wachezaji watatu kwenye tuzo ya Ballon d’Or kwenye kipindi cha miaka mitano ijayo.

FIFA YA FUATILIA KWA KARIBU KASHFA YA UPANGAJI MATOKEO

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA linafuatilia kwa karibu kashfa ya upangaji matokeo inayozikabili vilabu viwili vya soka vya ridhaa nchini Nigeria iliyotokea wiki iliyopita. Katika matokeo ambayo yanaonekana kama ya mchezo wa kriketi, klabu ya Plateau United Feeders iliibugiza Akurba FC kwa mabao 79-0 wakati Police Machine wao waliitandika Bubayaro FC kwa mabao 67-0 mwishoni mwa wiki iliyopita. Hatua uchunguzi kwa vilabu hivyo imekuja kutokana na timu hizo kuhitaji matokeo ya aina hiyo ili waweze kupanda daraja. Ambapo katika taarifa yake FIFA imedai kuwa inafuatilia tukio hilo la tmu hizo za Nigeria kwa karibu ili kuona jinsi gani Shirikisho la Soka la nchi hiyo, NFF litatatua tatizo hilo. FIFA inafanya hivyo kwa kutambua kuwa suala hilo ni la ndani hivyo NFF ina wajibu wa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua zinazostahiki kama ikigundulika aina yoyote ya udanganyifu katika mechi hizo.

TAIFA STARS SASA MMEIVA KUPAMBANA- TENGA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo wa kushindana katika mashindano yoyote, kwani tayari kimeiva.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye mechi zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast kimethibitisha hilo.
“Kiwango mlichoonyesha katika mechi hizo kila Mtanzania anayewafuatilia amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais Tenga na kuwataka kupigana kwa ajili ya Tanzania.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kesho (Julai 13 mwaka huu) saa 9 kamili alasiri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itacheza na Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Rais Tenga amesema TFF, mdhamini Kilimanjaro Premium Lager, Kamati ya Ushindi na Watanzania kwa ujumla wanawaunga mkono kwani wamekuwa wakiboresha kiwango chao kila wanavyozidi kucheza mechi tangu wake chini ya Kocha Kim Poulsen, Mei mwaka jana.
Wakati huo huo, Rais Tenga ameahidi kumpatia tiketi ya kwenda Uganda kwenye mechi ya marudiano mshabiki Wiseman Mwakyusa Luvanda anayetembea kwa miguu kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kesho.
“Kama ni kweli anakuja kwa kutembea, huyu ameonyesha kiwango kikubwa cha uzalendo kwa timu ya Taifa, nitampatia tiketi ya kwenda Kampala kuishangilia Taifa Stars kwenye mechi ya marudiano,” amesema Rais Tenga.

POULSEN, MICHO WATABIRI MECHI KALI
Makocha wa timu hizo Kim Poulsen wa Taifa Stars na Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwa vile kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo, makocha wote waliezea ubora wa wapinzani wao, lakini wakasisitiza kuwa wanaingia uwanjani kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa Kampala wiki mbili zijazo.
Kim alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa ubora wa viwango vya FIFA katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni changamoto kwao ingawa wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.
Naye Micho aliyefuatana na nahodha wake Hassan Wasswa alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini ya Kim, na itakuwa na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia wakati kwa upande wake atakuwa na wachezaji wawili tu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)