Kampuni ya vifaa vya
michezo ya Adidas imesimamisha mkataba wake wa udhamini na mwanariadha
nyota wa mbio fupi Tyson Gay wa Marekani baada ya kukutwa na
chembechembe za dawa za kuongeza nguvu. Msemaji
wa kampuni alidai kuwa awameshtushwa na tuhuma hizo kwa Gay na hata
kama bado hajakutwa na hatia ya kosa hilo moja kwa moja kampuni
itasimamisha udhamini wake mpaka hapo hukumu itakapotolewa. Gay
mwenye umri wa miaka 30, ndio mwanariadha wa pili mwenye kasi zaidi
duniani katika mbio za mita 100 akiwa sambamba na Yohan Blake wa Jamaica
na pia ndiye mwanariadha aliyeweka rekodi ya kasi zaidi kwa mwaka huu. Nyota
huyo ambaye aliwahi kuwa bingwa wa dunia katika mbio za mita 100, 200
na mita 400 kupokezana vijiti mwaka 2007 alishindwa kukata tuhuma hizo
na kudai kuwa alimwamini mtu ambaye alimwangusha na hivyo atapokea
adhabu yoyote atakayopewa.