CLUB ya Real Madrid ya
Hispania imetajwa kuwa klabu yenye thamani zaidi katika orodha ya timu
za michezo 50 zenye thamani zaidi duniani iliyotolewa na jarida Forbes
la nchini Marekani. Katika orodha hizo timu za Ligi Kuu ya Mpira wa Kimarekani-NFL ndizo zilizoonekana kutawala kwa kiasi kikubwa. Kwa
mujibu wa taarifa zilizochapishwa na jarida hilo Madrid ambao ni
mabingwa mara tisa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wana utajiri unaofikia dola
bilioni 3.3, utajiri huo ukiwa umeongezeka kwa dola bilioni 1.88
kulinganisha na mwaka uliopita baada ya kuongeza mapato yao kwa kuingia
mikataba na kampuni za Adidas na Shirika la Ndege la Emirates. Manchester
United wamepigwa kikumbo na Madrid na kushuka mpaka nafasi ya pili
wakiwa na utajiri wa dola bilioni 3.17 wakati mabingwa wa Hispania
Barcelona wao wamekwea kutoka nafasi ya tano mpaka ya tatu wakiwa na
utajiri unaofikia dola bilioni 2.6. Nafasi
ya nne inashikiliwa na timu ya Baseball ya Marekani ya New York Yankees
ambao wana dola bilioni 2.3, wakifuatiwa na Dallas Cowboys ya NFL dola
bilioni 2.1 na New England Patriots dola bilioni 1.6. Nyingine
ni Los Angeles Dodgers ya baseball dola bilioni 1.6, timu za NFL
Washington Redskins na New York Giant pamoja na klabu ya soka ya Arsenal
ya Uingereza ambazo zote hizo zina utajiri wa dola bilioni 1.3.