Shirikisho la Soka
Duniani-FIFA limedai kuwa klabu ya Coton Sport ya Cameroon haitaruhusiwa
kucheza mechi yao ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika mwishoni mwa wiki
hii kwasababu ya adhabu iliyopewa Shirikisho la Soka la nchi
hiyo-Fecafoot na FIFA. Hatua
ya kuzuiwa kwa klabu hiyo kunazidi kuleta utata katika michuano hiyo
mikubwa kabisa ya vilabu barani Afrika huku mahasimu wa soka nchini
Misri klabu ya Zamalek na Al Ahly ambao ndio mabingwa watetezi nao
wakiwa hawajui hatma ya mechi baina yao kwasababu ya vrugu za kisiasa
zinazoendelea nchini humo. Timu
nane zilizofanikiwa kuvuka hatua ya makundi, ndio zinatarajiwa kuchuana
kutafuta washindi watakaocheza nusu fainali ya michuano hiyo katika
mechi zao za kwanza mwishoni mwa wiki hii. FIFA
imesema kuwa tayari wameshaanza mazungumzo kujaribu kutatua mgogoro wa
Cameroon lakini mpaka sasa hakuna lolote lililofikiwa mpaka kuwashawishi
kuondoa adhabu ya kuifungia nchi hiyo kushiriki michuano yoyote ya
kimataifa waliyoitoa Julai 4 mwaka huu. Kufungiwa
kwa Cameroon kumekuja kufuatia uchaguzi wa Juni 19 ambao Mohammed Iya
alichaguliwa tena kuongoza Fecafoot pamoja na kukamatwa kwa tuhuma za
matumizi mabaya ya fedha wakati akiongoza kampuni ya Cotton Development
Corporation inayomiliki timu ya Cotton Sport.