Friday, July 19, 2013

MAELEZO YA SHUKURANI YA MWENYEKITI ALIYEMALIZA MUDA WAKE WA KAMATI YA UCHAGUZI YA TFF

1.Kama wote tunavyofahamu jana uongozi wangu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ulifikia tamati kama mlivyotangaziwa na Rais wa TFF. Kwa heshima kubwa naomba kutumia fursa hii kuwashukuru viongozi na wadau wa soka kwa ushirikiano mkubwa nilioupata kutoka kwao wakati nikitekeleza majukumu mbalimbali ya TFF.
 2. Kwa kushirikiana na viongozi wa mpira wa miguu katika TFF na mikoa yote Tanzania Bara, pamoja na wadau wa soka, nimepata fursa kulitumikia soka la nchi yetu kwa nafasi mbalimbali. Kwa pamoja tumetekeleza majukumu ya ujenzi wa misingi ya uongozi bora katika TFF na wanachama wake.
 3.Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF:
(i)kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, (Jan 2005 - Jan 2007). Nawashukuru pia wajumbe wa Kamati hiyo chini ya Mhe. Said El-Maamry kwa kunichagua kuwa Katibu wa Kamati hiyo. Ushirikiano mlionipatia ulioniwezesha kulitumikia taifa katika soka na kwa pamoja kurejesha nidhamu kwa kiwango kikubwa. (ii)kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu, iliyochunguza mkasa wa timu yetu ya Taifa ya wachezaji wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) mwezi Juni 2005. Nawashukuru wajumbe wa kamati  hiyo chini ya Dr. Hamad Ndee Mkuu wa Idara ya Michezo ya Chuo kikuu cha Dar es salaam, kwa kunichagua kuwa Katibu wa kamati hiyo iliyoandaa taratibu za mashindano ya vijana  ambazo ni msingi  wa mashindano ya vijana wa umri chini ya miaka 17  hapa nchini. 
(iii)kwa kuniteua kuwa Mjumbe wa Kamati Maalumu iliyotayarisha Programu ya kuendeleza Timu ya Taifa kwa kipindi cha miezi 15 (April 2006 hadi Juni 2007). Progamu iliyochangia Tanzania kiinua kiwango cha ubora wa soka kutoka nafasi ya 165 duniani mwezi Februari 2006 hadi nafasi ya 89 mwezi Desemba 2007.
 (iv)kwa kunipa fursa ya kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu ya kuboresha mapato ya TFF mwaka 2009. Nikiwa mjumbe na Katibu wa Kamati hiyo nilipata ushurikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa soka nchini  na nje ya nchi.  Nina imani kuwa TFF itakamilisha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati na ya wadau wa soka ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia tiketi za elektroniki.
 (v)kwa kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF  kwa  vipindi viwili; Februari 2009 - Machi 2011 na kuniteua tena kuiongoza Kamati hiyo kwa kipindi cha pili Machi 2011 hadi jana tarehe 18 Julai 2013. Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF kwa imani kubwa iliyoonyesha kwangu na wanakamati wenzangu.
4.Nawashukuru wajumbe wote wa wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa ushirikiano mkubwa mliotoa kwangu na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kushiriki kwa amani na utulivu na kuzingatia Katiba za vyama vyenu, Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi na hivyo kufanikisha zoezi la chaguzi za viongozi katika wilaya zote na Mikoa yote ya Tanzania Bara na hivyo kuwezesha kuwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu, ambao  katika kikao chake cha kwanza baada ya chaguzi hizo kimefanya jambo la kihistoria kuweka nguzo za  Mwenendo, Maadili  na Miiko ya uongozi wa soka la nchi yetu. Nilifarijika kuwa sehemu ya Mkutano Mkuu huo nikiwa mwalikwa.
5.Nawashukuru viongozi na wafanyakazi wote wa Sekretarieti ya TFF, wajumbe wa Kamati zote za TFF, Wajumbe wa Kamati zote za Uchaguzi za wanachama wa TFF na wanachama wao, kwa ushirikiano mkubwa na wa dhati uliowezesha kuwatumikia wadau wa soka kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
6.Nawashukuru sana wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ushirikiano niliopata kutoka kwao kwa muda tuliofanya kazi pamoja. Si jambo rahisi kusimamia chaguzi za mikoa yote na klabu zenye wanachama za Ligi Kuu, hata hivyo kwa kushirikiana na wadau mbalimali wa soka ambao nachukua fursa hii kuwashukuru, kwa pamoja tumeweza kutimiza jukumu hilo kikamilifu.  
7.Nawashukuru sana Wandishi na Wahariri wa habari za michezo na pia Wahariri Watendaji wa vyombo vya habari, kwa ushirikiano mzuri nanyi, ushirikiano na uhusiano wa uwazi ambao haukuwa na mikwaruzo ya aina yoyote kwa kipindi chote (Jan 2005-Jul 2013) tulichoshirikiana kwa pamoja kulitumikia soka la nchi yetu.
8.Namshukuru sana Rais wa TFF Ndg. Leodegar Tenga kwa imani kubwa aliyonayo kwangu na kwa wanakamati niliokuwa nao katika kutekeleza majukumu ya umma. Miaka ishirini na tisa (29) iliyopita nilipata fursa ya kufanya kazi ya mpira miguu kwa mara ya kwanza na Ndg. Tenga, nikiwa nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Chuo kikuu cha Dar es salaam, Desemba 1984, wakati Ndg. Tenga alipojitolea kuifundisha timu ya Chuo Kikuu cha DSM. Tangu wakati huo hadi sasa imani  na  ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya umma niliopata kutoka kwa Ndg. Tenga haujawai kutetereka hata kwa siku moja. Ni faraja kubwa kwangu kufanya kazi hizi za umma chini ya kiongozi anayeheshimika na kuaminika na wadau wa soka hapa nchini, Afrika Mashariki na Kati, Afrika na familia ya soka Duniani kwa ujumla. 
9.Mwisho, kwa viongozi na wadau wote wa mpira wa miguu, nawashukuru na nawatakia kheri, baraka  na mafanikio katika Uchaguzi Mkuu wa TFF na  ujenzi wa  soka la nchi yetu..
 Asanteni.
 Deogratias J. Lyatto
19 Julai 2013, Dar es salaam, Tanzania.

Wednesday, July 17, 2013

NURI SAHIN APATA FARAJA KWA USAJILI WA BORUSSIA DORTMUND"

Kiungo nyota wa Club ya Borussia Dortmund, Nuri Sahin ameonyesha furaha na shauku kwa usajili uliofanywa na klabu hiyo huku akiwa na matumaini ya kupiku utawala wa wapinzani wao Bayern Munich katika soka la Ujerumani. 
Ujio wa wachezaji kama Pierre-Emerick Aubameyang, Henrikh Mikhitaryan na Sokratis Papastathopoulous katika kikosi cha Jurgen Klopp kunategemewa kuisimamisha Bayern kurudia mafanikio ya kushinda mataji yote matatu nchini humo.  
Sahin, ambaye amebakisha miezi 12 ya mkopo kutoka klabu ya Real Madrid ana matumaini usajili huo unaweza kuwaongezea nguvu ili kupambana na Bayern ambao kwasasa wametawala soka la nchi hiyo. Dortmund walitolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na DFB-Pokal na Bayern msimu uliopita huku pia wakimaliza nyuma kwa alama 25 mbele ya Bayern ambayo ndio walikuwa mabingwa wa Bundesliga.

LIGI KUU NCHINI MISRI YAWEKWA KAPUNI KWA SABABU ZA KIUSALAMA"

Ligi Kuu ya kandanda nchini Misri imesimamishwa kwasababu za kiusalama kufuatia jeshi la nchi hiyo kumuondoa rais Mohamed Mursi madarakani mapma mwezi huu. Shirikisho la Soka la nchi hiyo lilitangaza rasmi kusitisha msimu wa ligi wa 2012-2013 huku kukiwa kumebaki mzunguko mmoja msimu kumalizika na timu nne kucheza hatua ya mtoano kwa ajili ya kumpata bingwa. Kwa zaidi ya wiki mbili toka jeshi limuondoe Mursi baada ya maandamano makubwa ya kumpinga, kumekuwa na vurugu huku watu zaidi ya saba wakiripotiwa kufa katika mapigano baina waislamu waliokuwa upande wa Mursi na wengine waliokuwa wakimpinga rais huyo. Hii ni mara ya pili katia kipindi cha miaka miwili ligi kusimamishwa katikati ya msimu baada ya mapema mwaka jana ligi hiyo kusitishwa tena kutokana na vurugu zilizotokea Port Said na kusababisha vifo vya mashabiki wapatao 74.

MARTINA ATARAJI KUREJEA TENA KAZINI KATIKA MCHEZO HUU"

Martina Hingis ambae ni mwanadada nyota wa tenisi wa zamani,  kutoka Switzerland anatarajiwa kurejea tena katika ulingo wa tenisi baada ya kustaafu mchezo huo mwaka 2007. Hingis mwenye umri wa miaka 32 amekubali mwaliko wa kucheza michuano ya wazi ya California ya wawili wawili akiwa sambamba na Daniela Hantuchova baadae mwezi huu. Nyota huyo ambaye amewahi kushinda mataji matano ya Grand Slam kwa mchezaji mmoja mmoja likiwemo taji la Wimbledon mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 16, Jumamosi iliyopita alichaguliwa kuwa mmoja wa wachezaji mashuhuri wa mchezo huo kuwahi kutokea. Akihojiwa kuhusiana na uamuzi huo wa kurejea uwanjani baada ya kupita kipindi kirefu, Hingis ambaye pia amewahi kushika namba moja katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanawake amesema bado anahisi kuwa na ari ya ushindani ndani ya nafsi yake. Mara ya kwanza Hingis alistaafu mchezo huo akiwa na miaka 22 baada ya kusumbuliwa na majeraha lakini alirejea tena mwaka 2006 kabla ya kustaafu tena mwaka 2007 baada ya kukutwa na chembechembe ya dawa za kusisimua misuli ingawa mwenyewe alikana tuhuma hizo.

CAF YATANGAZA KUSOGEZA MBELE MCHEZO WA LIGI YA MABINGWA KATI YA WATANI WA JADI"

Shirikisho la kandanda Barani Afrika-CAF limesogeza mbele mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika ambao unawakutanisha watani wa jadi nchini Misri timu za Zamalek na Al Ahly mpaka Jumatatu ijayo.  
Vigogo hao wa soka nchini humo walitarajiwa kucheza Jumapili katika mji wa El Gouna ambao uko kilometa 500 kutoka mji mkuu wa Cairo kutokana na sababu za kiusalama. Katika taarifa iliyotolewa katika mtandao wa Zamalek, wamethibitisha kuwa FIFA imekubali mchezo huo kuchezwa El Gouna pamoja na kwamba uwanja huo haukuwepo katika ratiba za michuano hiyo na kuamua kuchelewesha mchezo huo kwa siku moja kwasababu za kibiashara. Wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo ilikataa mapema kuhakikisha usalama wa mechi hiyo kuchezwa jijini Cairo au Alexandria kabla ya Zamalek kuchagua El Gouna.

WAKALA WA SUAREZ ASEMA KAMA KUNA CLUB INAMTAKA MCHEZAJI HUYO IWEKE MEZANI KITITA CHA NGUVU

Wakala wa mshambulaij  nyota wa klabu ya Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay" Luis Suarez’ amebainisha na kuweka wazi kama kuna klabu inahitaji kumsajili nyota huyo lazima iandae dau la nono la pauni miliaoni 40 ili kupata huduma yake.

Klabu ya Liverpool imesema itasikiliza ofa ya pauni milioni 40, lakini kuna uwezekano wa ofa hiyo kupanda mpaka kufikia pauni milioni 50 kumnunua nyota huyo mwenye matukio ya aina yake nchini England, likiwemo la kumng`ata beki wa Chelsea,  Ivanovic na kusimamishwa mechi kumi, pamoja na tuhuma za ubaguzi wa rangi kwa beki wa mabingwa wa soka nchini Englanda, Manchester United, Mfaransa Patrick Evra.

Wakala wa Suarez bwana Pere Guardiola, ambaye ni kaka yake kocha wa wekundu wa kusini mwa Ujerumani, The Bavarian, klabu ya Bayern Munich , Joseph Pep Guardiola , amasema atakaa mezani na klabu yoyote yenye uwezo wa kuweka mezani mzigo wa pauni milioni 40.

Ambapo sasa Baadhi ya Klabu kubwa barani Ulaya zinataka kuinasa saini ya Luis Suarez kutoka kwa majogoo wa jiji.

Arsenal ni klabu pekee yenye mpango wa nguvu zaidi kutaka kumsajili Suarez kwa pauni milioni 35, lakini ofa hiyo inaonkana haina maana kwa wekundu wa Anfield waliotangaza pauni milioni 40.

Awali Asernal walituma ofa ya pauni milioni 30, Liver wakatupilia mbali, wakaongeza tano, bado wakagomewa kabisa kwani wanataka 40 tu, huna mzigo huo basi amekosa huduma ya nyota huyo.

Saurez ambaye atajiunga na Liverpool waliopo  Melbourne jumatatu ijayo, ana mkataba na Liverpool mpaka mwaka 2016. Lakini Liver wameonekana kuwa na msimamo wa kumbakisha, huku klabu za Arsena, Real Madrid na Chelsea zakiimarisha rada zao kutaka kumsajili.

UONGOZI WA YANGA WAWATAKA MASHABIKI KUJITOKEZA KWA WINGI"

Club ya Yanga ya jangwani kupitia uongozi wake waumewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mechi ya kimataifa ya kirafiki itakayochezwa Julai 18 mwaka huu.
Mechi hiyo kimataifa ya Kirafiki dhidi ya timu ya 3 Pillars ya Nigeria inataraji kutimua vumbi Julai 18 mwaka huu katika uwanja wa Taifa.
Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya klabu zote mbili kabla ya ligi kuu kuanza mwezi ujao  ambapo Yanga pia inajinoa kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Mratibu wa mechi Salum Mkemi amesema kikosi cha wachezaji 17 na viongozi na makocha wao wapo jijini Dar es Salaam wakijifua kwa ajili mtanange huo utakaochezwa katika uwanja wa Taifa.
Mkemi amesema pia timu ya 3 Pillars ambayo imepanda daraja la ligi kuu nchini Nigeria inataraji kujipima na Coastal Union ya Tanga huku wakifanya mazungumzo na Mbeya City kwa ajili ya mechi nyingine za Kirafiki.
Katibu mkuu wa Yanga Lawrence Mwalusako amesema wachezaji wako kambini kujiwinda na michuano ya ligi kuu na kuongeza kuwa wana morali kuelekea mchezo huo.
Mratibu wa mechi ametangaza Viingilio vya mechi hiyo vitakuwa kati ya shilingi elfu tatu na elfu 15 ili kuwawezesha mashabiki wengi zaidi kuhudhuria kipute hicho.
Timu ya 3 Pillars inataraji kurejea nchini Nigeria Julai 30 mwaka huu.