Friday, June 14, 2013

MAKOCHA STARS, IVORY COAST ANA KWA ANA

Wakati timu ya Ivory Coast imewasili nchini jana usiku (Juni 13 mwaka huu) kwa ndege maalum, kocha wa timu hiyo Sabri Lamouchi na mwenzake wa Taifa Stars, Kim Poulsen watakutana na waandishi wa habari kuzungumzia mechi yao.

Mkutano huo utafanyika kesho (Juni 15 mwaka huu) saa 4 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mkutano huo pia utajumuisha makocha wa timu zote mbili. Ivory Coast inafanya mazoezi yake ya kwanza leo (Juni 14 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye viwanja vya Gymkhana.
Timu zote kesho (Juni 15 mwaka huu) zitafanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast watafanya mazoezi saa 9 kabla ya kuwapisha Stars saa 10 kamili. Maandalizi yanaendelea vizuri ikiwemo kuwasili kwa maofisa wote wa mechi itakayochezwa Jumapili saa 9 kamili alasiri.
Wakati huo huo, mauzo ya tiketi kwa ajili ya mechi hiyo yameanza leo mchana (Juni 14 mwaka huu) katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, City Sports Lounge iliyoko Mtaa wa Samora na Azikiwe, Dar Live Mbagala, BMM Salon iliyoko Sinza Madukani na Uwanja wa Taifa.
Mauzo yataendelea kesho katika vituo hivyo, wakati siku ya mchezo yatafanyika Uwanja wa Taifa. Viingilio katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika katika kundi C ni sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na VIP A sh. 30,000. Pia kuna kadi maalumu 100 kwa viti vya Wageni Maalumu (VVIP) zinazopatikana kwa sh. 50,000 katika ofisi za TFF.

TFF YATOA NOTISI YA MKUTANO MKUU
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa notisi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho utakaofanyika Julai 13 mwaka huu kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam ukiwa na ajenda moja ya marekebisho ya Katiba.
Notisi hiyo imetolewa juzi (Juni 12 mwaka huu). Rais ameitisha Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 25(1) ya Katiba ya TFF baada ya kupata maagizo kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa barua yake ya Aprili 29 mwaka huu.
Ajenda rasmi na taarifa nyingine zitatumwa kwa wajumbe siku 15 kabla ya Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 25(4) ya Katiba ya TFF. Wanachama wa TFF ambao ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu wanatakiwa kutuma majina ya wajumbe halali.
TFF inapenda kuwakumbusha wanachama wake kutuma majina ya wajumbe halali ili kufanikisha maandalizi ya Mkutano huo. Ni vizuri kuhakikisha kuwa jina linalotumwa ni la mjumbe halali wa Mkutano Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya TFF.
RCL YAINGIA HATUA YA TATU WIKIENDI HII
Mechi za kwanza za hatua ya tatu ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kuwania nafasi tatu za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao zinachezwa wikiendi hii kwenye viwanja vinne tofauti.
Mechi za kesho (Jumamosi) ni kati ya Kariakoo ya Lindi na Friends Rangers ya Dar es Salaam utakaochezwa katika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi wakati Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya wenyeji Kimondo SC na Njombe Mji.
Timu za Machava FC ya Kilimanjaro na Stand United FC ya Shinyanga, Polisi Jamii ya Mara na Katavi Warriors ya Katavi zilizokuwa zipambane kesho mechi zao zimesogezwa mbele hadi keshokutwa (Jumapili). Mechi hizo zimesogezwa kutokana na viwanja vya Ushirika mjini Moshi na Karume mjini Musoma kuwa na shughuli nyingine za kijamii.
Hata hivyo, TFF imesisitiza kuwa ikibainika kuwa viwanja hivyo havikutumika kwa shughuli za kijamii siku hiyo ya Jumamosi, hatua kali zitachukuliwa kwa wanachama wake (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa husika).
Mechi za marudiano za hatua hiyo ya tatu zitachezwa Juni 19 mwaka huu. Hatua ya nne ya RCL itachezwa kati ya Juni 23 na 23 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 29 na 30 mwaka huu.

RAMBIRAMBI MSIBA WA ABDALLAH MSAMBA



Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Pan Africans, Simba na Taifa Stars, Abdallah Msamba kilichotokea juzi usiku (Juni 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Msamba akiwa mchezaji, na baadaye kocha wa timu kadhaa alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha ikiwemo Villa Squad, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Msamba, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na klabu ya Villa Squad na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko ya mchezaji huyo yamefanyika leo (Juni 14 mwaka huu) katika makaburi ya Ndugumbi mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo wachezaji wa zamani na viongozi mpira wa miguu nchini. Mungu aiweke roho ya marehemu Msamba mahali pema peponi. Amina

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

BOLT AFANIKIWA KUREJESHA HESHIMA YAKE KUSHINDA MITA 200 ZA DIAMOND.


BAADA ya kushindwa katika mbio za mbio za mita 100 zilizofanyika jijini Rome wiki moja iliyopita bingwa mara sita wa medali za dhahabu za olimpiki, Usain Bolt amefanikiwa kurejesha heshima yake kwa kushinda mbio za mita 200 za Diamond League zilizofanyika jijini Oslo. Mara ya kwanza mbio hizo zilivurugika baada ya Churundy Martina kuanza kukimbia kabla ya wenzake hivyo kuenguliwa na mbio hizo kuanza tena ambapo Bolt alishinda kirahisi akiwaacha wenzake mbali kwa kutumia muda wa sekunde 19.79. 

Bolt amekuwa mwanariadha wa kwanza kukimbia chini ya sekunde 20 katika mbo za mita 200 msimu huu aliwasili jiji Oslo baada kushindwa na Justin Gatlin katika mbio za mita 100 zilizofanyika jijini Rome wiki iliyopita. Baadae Bolt aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa ingawa kulikuwa na baridi sana lakini alijitahidi kukimbia kwa kasi kadri alivyoweza na kama alivyoahidi hivyo anashukuru kwa kufanya vyema. Mshindi wa pili katika mbio hizo alikuwa ni Jasyma Saidy Ndure wa Norway huku mshindi wa tatu akiwa James Ellington wa Uingereza.

Thursday, June 13, 2013

PSG YAJIWEKA TAYARI KUPAMBANA NA MADRID KUHUSU BALE"

Mabingwa wa ligi kuu nchini ufaransa msimu huu Club ya Paris Saint-Germain-PSG inajiandaa kupambana na klabu ya Real Madrid katika kumuwania mshambuliaji nyota wa klabu ya Tottenham Hotspurs Gareth Bale anayekisiwa kuwa na thamani ya paundi milioni 85. Mabingwa hao wa ligi nchini Ufaransa wanataka kumchukua meneja Spurs Andres Villas-Boas ili aweze kumshawishi nyota huyo kumfuata kwenda huko. Hatahivyo, hata kama Villas-Boas akiamua kubakia jijini London, hilo haliwezi kuzuia nia ya klabu hiyo tajiri nchini Ufaransa kuvunja benki na kumsajili mchezaji huyo kwa dau kubwa. PSG imetumia zaidi ya paundi milioni 200 katika usajili wa nyota mbalimbali kuanzia mwaka 2011 wakati Kampuni ya Michezo inayosimamiwa na familia ya kifalme ya Qatari ilipoinunua klabu hiyo. Kwasasa PSG wameshakubali kuwa lazima wavunje rekodi ya usajili kama wanataka kumng’oa nyota huyo kutoka Tottenham, rekodi ambayo bado inashikiliwa na Cristiano Ronaldo ambaye Real Madrid walimnunua kwa paundi milioni 80 kutoka Manchester United.

LAPORTA AMKINGIA KIFUA MKALI WA DUNIA -MESSI

RAIS wa zamani wa mabingwa wa Hispania, Barcelona Joan Laporta amemkingia kifua nyota wa klabu hiyo Lionel Messi dhidi ya tuhuma za ukwepaji kodi zinazomkabili. Laporta ambaye ameiongoza Barcelona kuanzia mwaka 2003 mpaka 2010 aliiambia radio moja nchini humo kuwa ana uhakika kuwa si Messi wa baba yake wamefanya kitedo hicho. Messi na baba yake Jorge wameshitakiwa na jana na mwendesha mashtaka Raquel Amado wa mji wa Gava uliopo karibu na Barcelona ambapo anaishi nyota huyo, kwa kosa kukwepa kodi inayofikia kiasi cha euro milioni 4.1 kati ya mwaka 2007 na 2009. Laporta amesema hakumbuki katika kipindi chake chote cha uongozi kama nyota huyo alikuwa akijishughulisha na makampuni yasiyo halali, na anachojua yeye Messi aliyofautiana na mmoja wa washauri wake hivyo anadhani tuhuma hizo zimetoka huko.

FABREGAS AKANUSHA TUHUMA ZA KUREJEA JIJINI LONDON.

KIUNGO nyota wa klabu ya Barcelona Cesc Fabregas amekanusha  na kutanabaisha kuwa tuhuma  za kwamba anataka kurejea jijini London nchini Uingereza baada ya kukosa namba ya kudumu katika klabu hiyo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, alijiunga na Barcelona mwaka 2011 lakini Manchester United na klabu yake ya zamani ya Arsenal wanaaminika kutaka kumchukua mchezaji huyo kutoka Camp Nou. Fabregas amesema siku zote amekuwa na furaha Barcelona na yoyote anayesema kwamba anataka kuondoka hamjui na hajawahi kuzungumza nae.
Kiungo huyo ametokea katika shule ya vipaji ya Barcelona akiwa na miaka 10 mpaka 16 alisajiliwa na Arsenal, na ameichezea klabu hiyo mechi 303 kwa kipindi cha miaka nane na kufanikiwa kufunga mabao 57.

TIKETI MECHI YA STARS KUANZA KUUZWA KESHO

Wakati timu ya Ivory Coast inatarajiwa kuwasili leo usiku (Juni 13 mwaka huu) kwa ndege maalum, tiketi kwa ajili ya mechi kati yake na Taifa Stars itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa zinaanza kuuzwa kesho mchana (Juni 14 mwaka huu) kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam. Vituo vitakavyotumika kwa mauzo hayo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani. Viingilio katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika katika kundi C ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani, sh. 7,000 viti vya rangi ya bluu, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000. Pia viti 100 vilivyo katika sehemu ya Wageni Maalumu (VVIP) vitauzwa kwa sh. 50,000 kila kimoja. Tiketi hizo zitauzwa katika ofisi za TFF, na watakaonunua watapewa kadi maalumu zenye majina yao, majina ambayo pia watayakuta katika vita watakavyokaa. Kwa maana hiyo hakutakuwa pasi maalumu (free pass) za kuingia VVIP.

PONGEZI KWA RAIS MPYA WA ZFA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amempongeza Rais mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Ravia Idarous Faina aliyechaguliwa katika uchaguzo mdogo uliofanyika hivi karibuni. Amesema ushindi aliopata Faina unaonyesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA walivyo na imani naye katika kuhakikisha maendeleo ya mpira wa miguu visiwani humo. Rais Tenga amesema ni imani yake kuwa Rais Faina ataendeleza ushirikiano uliopo kati ya TFF na ZFA kwa ajili ya ustawi wa mpira wa miguu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumtakiwa kila kheri katika wadhifa wake huo mpya.

WAAMUZI WATATU WAFUNGIWA MIEZI MITATU

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefungia miezi mitatu waamuzi watatu walioshindwa kuchezesha mechi namba 32 ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Mpwapwa Stars ya Dodoma na Machava FC ya Kilimanjaro iliyokuwa ichezwe Juni 2 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. TFF kupitia Kamati yake ya Waamuzi iliyokutana katika kikao chake cha Juni 12 mwaka huu kupitia taarifa mbalimbali za waamuzi wa RCL ilibaini makosa yaliyofanywa na baadhi ya waamuzi na kuyatolea uamuzi. Waamuzi hao waliofungiwa ambao wanatoka mkoani Singida ni Jilili Abdallah, Amani Mwaipaja na Theofil Tegamisho. Wamefungiwa kwa kutoripoti katika kituo walichopangiwa (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma) na kutoa taarifa ya uongo kwa kushirikiana na Kamishna wa mechi hiyo. Kanuni iliyotumika kuwafungia ni ya 28 kifungu (d) na (g) ya Ligi za TFF, na adhabu hiyo imeanza Juni 13 mwaka huu. Waamuzi hao pamoja na kamishna badala ya kwenda Uwanja wa Jamhuri, wao walikwenda kwenye Uwanja wa Mgambo ulioko Mpwapwa na kuandika ripoti iliyoonesha kuwa timu ya Machava FC haikufika uwanjani wakati wakijua kuwa mechi hiyo ilitakiwa kuchezwa katika Uwanja wa Jamhuri.

TAFAKARI YA LEO BARCA ILIVYOFANYA JEURI KUMTAFUTIA MESSI COMBINATION JE KWA NEYMA ITAKUWAJEEEE??

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Barcelona imetumia jumla ya Euro 205 milioni kwa ajili ya kusaka mshambuliaji ambaye anaweza kumpunguzia Messi mzigo wa ustaa alioubeba kwa muda mrefu klabuni hapo.
Hivyo kuwasili kwa mshambuliaji wa Santos na timu ya taifa ya Hispania, Neymar, katika kikosi cha Barcelona, inamaanisha kuwa Barcelona imeendelea kutumia fedha nyingi kusaka mshambuliaji ambaye anaweza kung’ara vyema kwa pamoja na staa wao, Lionel Messi.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Barcelona imetumia jumla ya Euro 205 milioni kwa ajili ya kusaka mshambuliaji ambaye anaweza kumpunguzia Messi mzigo wa ustaa alioubeba kwa muda mrefu klabuni hapo.
Thierry Henry
Katika msimu wake wa kwanza tu ndipo Henry alifikia matarajio ya mashabiki wa Barcelona. Baadaye kuibuka kwa kinda wa Kihispaniola, Pedro Rodriguez, kulimfanya Henry apate nafasi finyu ya kucheza katika kikosi cha kwanza na mwisho aliamua kutimkia Marekani katika klabu ya New York Bulls.
Hata hivyo Henry hakufikia kiwango alichokuwanacho wakati anachezea Arsenal chini ya Arsene Wenger ingawa katika kipindi chake na Barcelona alishinda mataji kadhaa.
Zlatan Ibrahimovich
Ukitazama hapa katika hali ya kawaida kilikuwa kipindi kibaya katika harakati za maisha ya soka ya Ibrahimovich. Tofauti na matarajio ya wengi, licha ya kusajiliwa kwa Euro 46 milioni huku pia Barcelona wakimtoa  Samuel Eto’o kwenda Inter Milan, bado Ibrahimovich hakutamba sana Nou Camp.
Mwishowe alijikuta akiingia katika mgogoro mkubwa na kocha wa wakati huo, Pep Guardiola. Ibrahimovich alimshutumu Guardiola kwamba alikuwa anampendelea zaidi Messi huku wakati mwingine akimchezesha nafasi ya kati wakati yeye yuko benchi.
Baada ya msimu mmoja tu, Zlatan aliondoka akarudi Italia ambako alijiunga na AC Milan.
David Villa
Alionekana mmoja kati ya wachezaji ambao wangeweza kumpunguzia mzigo wa mabao staa huyu wa Argentina. Alianza vema, lakini baadaye aliumia katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia, ilikuwa Desemba 2011.
Mbali na hilo tangu hapo kasi yake imepungua uwanjani na sasa inasemekana ataondoka zake Barcelona katika kipindi hiki cha uhamisho wa wachezaji.