Mabingwa wa ligi kuu nchini ufaransa msimu huu Club ya Paris
Saint-Germain-PSG inajiandaa kupambana na klabu ya Real Madrid katika
kumuwania mshambuliaji nyota wa klabu ya Tottenham Hotspurs Gareth Bale
anayekisiwa kuwa na thamani ya paundi milioni 85. Mabingwa
hao wa ligi nchini Ufaransa wanataka kumchukua meneja Spurs Andres
Villas-Boas ili aweze kumshawishi nyota huyo kumfuata kwenda huko. Hatahivyo,
hata kama Villas-Boas akiamua kubakia jijini London, hilo haliwezi
kuzuia nia ya klabu hiyo tajiri nchini Ufaransa kuvunja benki na
kumsajili mchezaji huyo kwa dau kubwa. PSG
imetumia zaidi ya paundi milioni 200 katika usajili wa nyota mbalimbali
kuanzia mwaka 2011 wakati Kampuni ya Michezo inayosimamiwa na familia
ya kifalme ya Qatari ilipoinunua klabu hiyo. Kwasasa
PSG wameshakubali kuwa lazima wavunje rekodi ya usajili kama wanataka
kumng’oa nyota huyo kutoka Tottenham, rekodi ambayo bado inashikiliwa na
Cristiano Ronaldo ambaye Real Madrid walimnunua kwa paundi milioni 80
kutoka Manchester United.