
Stars ambayo iliwasili ikitokea jijini
Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi hiyo
itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakwenda Afrika Kusini
mwakani imefikia hoteli ya Mt. Zion iliyoko eneo la Kisseka katikati ya
Jiji la Kampala.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars inayodhaminiwa
na Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen ameridhishwa na kiwango cha
hoteli hiyo, kwani ndiyo ambayo timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro
Stars) ilifikia Novemba mwaka jana ilipokuja Kampala kushiriki michuano
ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Stars ambayo ilitiwa chachu na Rais
Jakaya Kikwete alipokutana nayo Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati
ikiondoka kuja Kampala, na kuitakia kila la kheri itafanya mazoezi yake
ya mwisho kesho (Julai 26 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kujiandaa kwa
mechi ya Jumamosi.
Kocha Kim amesema ingawa mechi hiyo ni
ngumu, lakini kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwani wachezaji
wako wako vizuri na ari kwa ajili ya mechi iko juu.
Wachezaji wote wako katika hali nzuri,
isipokuwa Khamis Mcha aliyekuwa na maumivu ya goti, lakini kwa mujibu wa
madaktari wa timu anaendelea vizuri kwani tayari wanampa mazoezi
mepesi.
Kikosi cha kamili cha Stars ilichoko
hapa kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki
ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir
Haroub na Vincent Barnabas.
Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd,
Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum
Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na
Mrisho Ngasa.
Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen
atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari siku ya Jumatatu (Julai 29
mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa
mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)