Mchezaji tenisi nyota
Rafael Nadal amefanikiwa kutawadhwa bingwa mpya wa michuano ya Kombe la
Rogers baada ya kugaragaza Milos Raonic wa Canada. Nadal mwenye umri wa
miaka 27 kutoka Hispania alitumia dakika 68 pekee kushinda mchezo huo
kwa 6-2 6-2 na kunyakuwa taji lake la nane kwa mwaka huu. Toka arejee
tena uwanjani Februari mwaka huu baada ya kupona majeraha, Nadal
amefanikiwa kushinda michezo 48 kati ya 51 aliyocheza na kufanikiwa
kushinda taji lake la nane katika michuano ya wazi ya Ufaransa. Kwa
upande wa wanawake mwanadada anayeshika namba moja katika orodha za
ubora Serena Williams wa Marekani naye alifanikiwa taji la michuano hiyo
kwa kumgaragaza Sorana Cirstea wa Romania. Williams mwenye umri wa
miaka 31 alihitaji dakika 65 pekee kummaliza mpinzani wake kwa 6-2 6-0
na kunyakuwa taji hilo kwa mara ya tatu.