Thursday, July 4, 2013

ROONEY ATAKIWA KUWA SILISHA BARUA KWA MAN U

MSHAMBULIAJI Wayne Rooney atatakiwa kuwasilisha barua ya maandishi ya kuomba kuondoka ikiwa anataka kuachana na  Manchester United.
Mpachika mabao huyo wa Old Trafford, alirejea mazoezini jana huku mustakabali wake ukiwa bado haueleweki. Imefahamika hakuwa na Mkutano mahsusi na kocha mpya David Moyes juu ya suala lake. 
Hilo linaweza kutokea katika kituo cha mazoezi cha klabu, Carrington leo. Wawili hao walizungumza jana, lakini si kwa muda mrefu na msimamo wa United kwake bado haujabadilika.

Hajielewi: Mustakabali wa Wayne Rooney bao haueleweki licha ya jana kurejea mazoezini
Wamesema mshambuliaji huyo wa England hauzwi. Kuhusu tetesi za wapinzani wao katika Ligi Kuu, Arsenal kutaka rasmi kumsajili tangu wiki iliyopita, United bado haijawasiliana na yoyote anayemtaka Rooney.
Sakata hili linaweza kugeuka tu iwapo mshambuliaji mwenyewe ataamua kulazimisha kuondoka. BIN ZUBEIRY iliandika mwishoni mwa msimu uliopita kwamba, Rooney aliomba kuondoka kwa kocha aliyestaafu, Sir Alex Ferguson.
Ombi la kuondoka litamaanisha Rooney hatadai chochote katika Mkataba wake wa miaka miwili uliobakia ambao alikuwa analipwa Pauni 250,000 kwa wiki.

Moyes, bado anataka kumuongeza katika benchi lake la ufundi, beki wa zamani wa United, Phil Neville na ni matumaini Rooney atakubali kubaki msimu ujao kufanya na kazi na kocha wa zamani wa Everton, aliyeinua kipaji chake Goodison Park.
Huku Moyes akitarajiwa kuzungumza na Waandishi wa Habari kwa mara ya kwanza kesho, ufafanuzi utakuja muda si mrefu.

Harudi: Angalau bado, kwa Cristiano Ronaldo
Wakati huo huo, mchezaji mwenzake wa zamani Rooney, Mreno Cristiano Ronaldo ameendelea kuweka wazi juu mapenzi yake na United. Mshambuliaji huyo wa Real Madrid  amesema jana kwamba anataka kurudi Ligi Kuu, lakini hakusema lini.
"Nalikosa kweli soka la England. Kwangu ilikuwa moja ya miaka bora katika maisha yangu ya soka wakati nipo huko Manchester United. Ni klabu ambayo bado ipo moyoni mwangu. naikosa kweli kweli. Lakini kwa sasa maisha yangu yapo Hispania. Nafurahia kucheza huko pia. Mustakabali hatuwezi kuujua,"alisema Ronaldo.

ISCO ASEMA LENGO KUU NI KUISAIDIA MADRID KUTWAA UEFA

Baada ya kusajiliwa katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi na club ya Real Madrid Isco ametanabaisha na kusama kuwa lengo lake kubwa ni kukisaidia kikosi cha timu hiyo kinachonolewa na kocha Carlo Ancelotti kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kocha aliyeoondoka Jose Mourinho ameinoa klabu hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu na kuisadia klabu hiyo kufika nusu fainali ya ligi hiyo mara tatu lakini bado wamekuwa na kiu ya muda mrefu ya kulisubiria taji lao 10 katika michuano hiyo. Akijiunga na Madrid kwa mkataba wa miaka mitano kutokea Malaga, Isco sasa ana malengo ya kuiwezesha klabu hiyo kuendeleza historia yake kwa kunyakuwa taji hilo mapema iwezekanavyo. Akihojiwa katika utambulisho rasmi, Isco amesema watu wote wanahusiana na klabu hiyo wamekuwa na kiu ya taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na ni mategemeo yake kwamba msimu unaokuja taji hilo litatua Santiago Bernabeu.

GIGGS NAYE AWA KOCHA MCHEZAJI SAFU YA BENCH LA UFUNDI.

KLABU ya Manchester United imemtangaza kiungo wake mkongwe Ryan Giggs kuwa kocha mchezaji wa klabu hiyo. Giggs mwenye umri wa miaka 39, aliongeza mkataba wa mwaka mmoja Machi mwaka huu na sasa ataunganisha na majukumu yake mapya yA Kocha mchezaji wa kikosi cha kwanza cha United. Katika taarifa yake Moyes amesema amefurahishwa na Giggs kuikubali nafasi hiyo ya kuwa mchezaji na pia kocha na uzoefu wake wakipindi kirefu utasaidia kuifanya United kuendeleza ubora wake. Giggs ambaye ni raia wa Wales alianza kuchomoza katika timu ya wakubwa ya United mwaka 1991 na kufanikiwa kushinda mataji 13 ya Ligi Kuu nchini Uingereza, manne ya Kombe la FA na medali mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
RYAN GIGGS NA MAN U
-UMRI: 39
-MECHI: 941
-MAGOLI: 168
-MATAJI YA LIGI: 13
-FA CUP: 4
-LIGI CUP: 4
-UEFA CHAMPIONZ LIGI: 2

HISPAIN BADO NAMBARI MOJA DUNIANI VIWANGO VYA FIFA

LICHA wa kutandikwa na Brazil katika  Michuano ya Kombe la Mabara hatua ya fainali Mabingwa wa Dunia Spain bado wameendelea kukamata Nambari moja katika Listi ya FIFA ya Ubora Duniani iliyotoka leo huku Brazil wakipanda Nafasi 13 na kushika Nafasi ya 9 lakini England  imeporomoka Nafasi 6 hadi kufikia Namba 15 na Tanzania imeshuka Nafasi 12 na sasa ipo ya 121.
Ivory Coast ndiyo Nchi ambayo iko juu kupita zote Afrika na inakamata Nafasi ya 13.
Brazil, ambao Jumapili iliyopita walitwaa Kombe la Mabara, wamerudi 10 Bora na sasa wapo Nafasi ya 9.
Listi nyingine itatolewa Agosti 8.
20 BORA:
Spain
Germany
Colombia (Imepanda Nafasi 4)
Argentina (Imeshuka 1)
5 Holland
Italy (Imepanda 2)
Portugal (Imeshuka 1)
Croatia (Imeshuka 4)
9 Brazil (Imepanda 13)
10 Belgium (Imepanda 2)
11 Greece (Imepanda 5)
12 Uruguay (Imepanda 7)
13 Ivory Coast
14Bosnia-Herzegovina (Imepanda 1)
15 England (Imeshuka 6)
16Switzerland (Imeshuka 2)
17 Russia (Imeshuka 6)
18 Ecuador(Imeshuka 8)
19 Peru (Imepanda 11)
20 Mexico (Imeshuka 3).

WACHINA WAKABIDHI UWANJA WA TAIFA KWA SERIKALI.

UWANJA_WA_TAIFA_DARSerikali ya Tanzania hatimaye imekabidhi Uwanja wa Taifa wa Jijini Dar es Salaam na wachina ikiwa ni awamu ya Kwanza.
Makabidhiano hayo ya Uwanja huo uliochukua Miaka 7 kujengwa yalifanyika Jana kwa kutia saini na kubadilishana Vyeti kati ya Balozi wa China Nchini Tanzania, Li Youqing, na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Sihaba Mkinga.
Akizungumza, Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr. Fenella Mukangara, aliishukuru China kwa msaada wao mkubwa wa Fedha na Ujenzi.
Pia, Waziri Mukangara, alisifu Usimamizi wa China wa Uwanja huo tangu ujenzi ulipokamilika na tangu Uwanja huo ulipofunguliwa rasmi hapo Tarehe 25 Februari 2009 na Rais wa zamani wa China, Hu Jintao, na Rais Jakaya Kikwete.
Uwanja wa Taifa, unaochukua Washabiki 60,000 wote wakiwa Vitini, umegharimu Shilingi Bilioni 56 na kati ya hizo China ilitoa Bilioni 33.4 na Tanzania ilitoa Fedha zilizobaki.
Uwanja huu ni wa kisasa na upo katika Viwango vinavyokubalika na FIFA na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki.
Serikali imedokeza kuwa hivi sasa wapo kwenye mazungumzo ya kutafuta Fedha ili kugharamia Ujenzi wa Awamu ya Pili na inatarajiwa Serikali ya China itahusishwa na pia Mkandarasi aliejenga Awamu ya Kwanaza, Beijing Construction Engineering Company Limited, ndio watashughulikia Awamu hii.
Baada ya kukamilika kwa Ujenzi wa Awamu ya Pili, Tanzania itakuwa iko tayari kuwa Mwenyeji wa Mashindano makubwa ya Michezo ya kila aina.

CHELSEA YAFIKIA MAKUBALIANO NA MARCO VAN GINKEL WA VITESSE FC YA UHOLANZI".

WAKALI wa Darajani Club ya soka ya Chelsea imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa klabu ya Vitesse Arnhem ya Uholanzi, Marco van Ginkel. Kiungo huyo mwenye miaka 20 ambaye ametokea katika shule ya watoto ya Vitesse kabla ya kupata namba katika kikosi cha kwanza April mwaka 2010 atajiunga na Chelsea baada ya kukamilisha taratibu za vipimo vya afya. Van Ginkel amekuwa akicheza katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 21 ya Uholanzi na mara moja ameshaitwa katika kikosi cha timu ya wakubwa akiingia kama mchezaji wa akiba katika mchezo dhidi ya Ujerumani Novemba mwaka jana. Kiungo huyo anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na meneja mpya wa Chelsea Jose Mourinho kufuatia kusajiliwa kwa mshambuliaji Andre Schuerrle ktoka Leverrkusen mwezi uliopita.

YONDAN AWA MCHEZAJI BORA WA LIGI KUU TZ 2012-2013

INJINI ya Yanga Sc beki Kevin Patrick Yondan amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 na kuzawadiwa kitita cha Sh. Milioni 5. Hata hivyo, katika hafla ya kutoa zawadi za washindi wa Ligi Kuu msimu uliopita kutoa wadhamini, Vodacom Tanzania zilizofanyika katika hoteli ya Double Tree, Dar es Salaam jana usiku, Yondan hakuwepo na tuzo yake alipokelewa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto, kutoka kwa mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara. Yondan ambaye alikuwa katika msimu wake wa kwanza Yanga SC, yuko kwenye kambi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa na mchezo dhidi ya Uganda Julai 13, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kipa chipukizi wa Tanzania Prisons FC ya Mbeya, David Burhan alishinda tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu na kupewa Sh. Milioni 5, wakati mfungaji bora, Kipre Herman Tchetche raia wa Ivory Coast wa Azam FC alipewa Milioni 5 pia na Fully Maganga wa JKT Mgambo alipewa tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu na kuzawadiwa Milioni 5. Kocha mpya wa Simba, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ ameshinda tuzo ya kocha bora kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa na Kagera Sugar msimu uliopita na kuzawadiwa Milioni 7.5 sawa na refa bora, Simon Mbelwa. Yanga SC pamoja na kuzawadiwa Sh. Milioni 70 za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, waliongezewa Milioni 15 kwa kuwa timu yenye nidhamu zaidi kwenye ligi hiyo msimu uliopita, hivyo kuondoka na jumla ya kiasi cha Sh. Milioni 85. Azam FC washindi wa pili kwa msimu wa pili mfululizo, walizawadiwa Sh. Milioni 35, Simba SC washindi wa tatu Milioni 25 na Kagera Sugar washindi wa nne walipewa Milioni 20. Kwa upande wa zawadi za wachezaji wa timu za vijana za klabu za Ligi Kuu, Hamisi Saleh (JKT Ojoro), Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Chande Magoja (Mgambo JKT), Tonny Kavishe (Mgambo JKT) na Rajab Zahir (Mtibwa Sugar), wote wamezawadiwa Sh. Milioni 1 kila mmoja. Zawadi za wachezaji wa timu za vijana, walizozawadiwa kwa kuzichezea mechi nyingi timu zao za wakubwa katika Ligi Kuu, zimetoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Rajab Zahir amesaini Yanga SC na tayari amejiunga nayo.