Tuesday, August 13, 2013

ARSENAL YAFIKIA ASILIMIA 99 KUMNASA GUSTAVO

Kiungo mahiri wa kimataifa wa Brazil, Luiz Gustavo anatarajiwa kukubali uhamisho wake kwenda Arsenal ili aweze kucheza zaidi katika kikosi cha kwanza kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil. Kiungo huyo mkabaji wa Bayern Munich ambaye amejikuta akishindwa kupata namba ya moja kwa moja katika kikosi cha kwanza anakaribia kukamilisha usajili wake wa paundi milioni 14 kwenda Emirates wiki hii. Gustavo anaamini kuwa nafasi yake itazidi kuwa finyu chini ya kocha mpya Pep Guardiola ambaye ameonyesha kumtumia sasa Javi Martinez ambaye naye anacheza nafasi hiyo ndio maana anaona uhamisho wake kwenda Arsenal unaweza kumsadia. Akihojiwa jijini Basel kabla ya mchezo wa kirafikiwa kimataifa baina ya Brazil na Switzerland kesho, Gustavo amesema mkataba wake na Bayern unamalizika 2015 lakini ni muhimu kwake kucheza katika kikosi cha kwanza ili aweze kuitwa katika timu ya taifa.

NASRI AOMBA RADHI KUHUSU TABIA YAKE YA LAKINI ASEMA HAJAUWA MTU

Kiungo nyota wa kimataifa wa Ufaransa, Samir Nasri ameomba radhi kwa tabia yake lakini amesisitiza kuwa hajaua mtu hivyo anapaswa kupewa nafasi nyingine ya kujirekebisha. Kiungo huyo anayecheza katika klabu ya Manchester City alifungiwa mechi tatu na Shirikisho la Soka la Ufaransa kufuatia kumtukana mwandishi katika michuano ya Ulaya 2012 na hajaitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo toka kipindi hiko. Hatahivyo Nasri sasa yuko tayari kurejea katika mchezo wa kirafiki kati ya Ufaransa na Ubelgiji baada ya kocha Didier Deschamps kuridhishwa na tabia ya mchezaji huyo. Nasri mwenye umri wa miaka 26 aliomba radhi kwa tukio alilofanya katika michuano hiyo mwaka jana na kudai kuwa angetakiwa kukabiliana na tatizo hilo kwa weledi zaidi kuliko alivyofanya. Nyota aliendelea kudai kuwa anashukuru kupewa nafasi nyingine ya kujirekebisha na ana mategemeo yaliyotokea hayatajirudia kwasababu hivi sasa anajua jinsi gani ya kumudu hasira zake tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

KAMATI KUTANGAZA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF

Mchakato wa uchaguzi wa kamati mpya ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unatarajiwa kutangazwa kesho (Agosti 13 mwaka huu).
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Hamidu Mbwezeleni atakutana na Waaandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF saa 6 kamili mchana ambapo mbali ya mchakato utakavyokuwa anatarajia kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi huo ambao awali ulitarajiwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilikutana Jumapili (Agosti 11 mwaka huu) na inatarajia kuwa na kikao kingine leo (Agosti 12 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine itazungumzia maandalizi ya uchaguzi huo.
Mbali ya Mbwezeleni, wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Moses Karuwa (Makamu Mwenyekiti), Mohamed Sinani, Chabanga Dyamwale na Kitwana Manara.

MAGORI, LINA WAINGIA KAMATI ZA CAF
Watanzania Crescentius Magori na Lina Kessy wameteuliwa kuwa wajumbe kwenye kamati ndogondogo (standing committees) mpya za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) zilizotangazwa juzi na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Hicham El Amrani.
Magori na Lina ambao ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF watakuwa kwenye kamati hizo kwa kipindi cha miaka miwili (2013-2015). Magori ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Mpira wa Miguu wa Ufukweni (Beach Soccer) wakati Lina ameingia kwenye Kamati ya Maandalizi ya Mpira wa Miguu kwa Wanawake.
Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani ameteuliwa tena kuwemo kwenye Bodi ya Rufani ya CAF yenye wajumbe 12 kwa kipindi kingine cha miaka miwili. Nyamlani alikuwepo kwenye bodi iliyopita, na itaendelea kuwa chini ya uenyekiti wa Prosper Abega kutoka Cameroon.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF yuko kwenye kamati tano za Shirikisho hilo. Kamati hizo ni Kamati ya Fedha ambayo ni Makamu Mwenyekiti na Kamati ya Maandalizi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Kamati nyingine ni Kamati ya Masoko na Televisheni ambayo ni Mwenyekiti, Kamati ya Ufundi na Maendeleo, na Kamati ya Ushauri na Vyama Wanachama wa CAF.

KAMATI YA SHERIA KUPITIA USAJILI
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inakutana leo jioni (Agosti 13 mwaka huu) na kesho (Agosti 14 mwaka huu) kupitia na kufanyia uamuzi usajili wa wachezaji wenye matatizo.

Hatua ya kwanza ya usajili imeshamalizika wakati hatua ya pili ya usajili inaanza kesho (Agosti 14 mwaka huu) ikihusisha wachezaji ambao watakuwa hawajasajiliwa katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu na wale kutoka nje ya Tanzania.

Hivyo, dirisha la uhamisho kwa wachezaji wa kimataifa litafungwa baada ya hatua ya pili ya usajili kumalizika Agosti 29 mwaka huu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Monday, August 12, 2013

LOPEZ AONYESHA KIWANGO CHA JUU ZAIDI KATIKA NAFASI YAKE"

Kipa mahiri wa Real Madrid Diego López ameweka katika wakati mgumu  kocha wake Carlo Ancelotti.   
Ancelotti anaonekana kuingia katika wakati mgumu kutokana na namna Lopez kuonyesha kiwango cha juu.
 
Lopez ameonyesha kiwango cha juu katika mechi za kirafiki za timu hiyo ambazo imecheza.


Hali inayomfanya Ancelotti azidi kuchanganyikiwa kuwa yupi hasa awe kipa namba moja kati ya hao wawili.
Lopez alianza kupata nafasi ya kudaka baada ya kocha wa zamani wa Real Madrid, Jose Mourinho kukorofishana na Casillas.


KOCHA MPYA WA BARCA ASEMA BADO KIKOSI CHANGU HAKIJA KIDHI HITAJI LANGU

Meneja mpya Barcelona, Gerardo Martino amekiri kuwa kikosi chake bado hakijawa katika hali anayoitaka.
“Kweli tumecheza na kushinda katika mechi za majaribio, lakini kiwango haikuwa kizuri.
“Hata mashabiki waliokuja katika mechi zetu watakubaliana nasi kwamba hatukuwa katika fomu nzuri.  
“Lakini tutajipanga, mambo yatakuwa tifauti tutakapoanza msimu na mechi yetu na Levante hakika tutafanya vizuri sana,” alisema kocha huyo maarufu Tata.
Kocha huyo amechukua nafasi ya Tito Vilanova ambaye ameshindwa kuendelea na kazi kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa kansa.

AZAM FC YAMALIZA ZIARA YAKE NCHINI AFRIKA KUSINI KWA KIPONDO

Kikosi kabambe cha azam fc
Washindi wa pili mfululizo wa ligi kuu vodacom tanzania bara Azam FC leo imekamilisha ziara yake ya Afrika Kusini kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Moroka Swallows katika dimba la Uwanja wa Volkswagen Dobsonville mjini Soweto.
 
Aidha Katika Ziara hiyo huo unakuwa mchezo wao wa tatu kuambulia kipigo baada ya awali kuchapwa 3-0 na Kaizer Chiefs, 2-1 na Orlando Pirates.

Hata hivyo katika ziara hiyo wanarambaramba hao wamefanikiwa kuibuka na ushindi mchezo mmoja dhidi ya Mamelodi Sundowns baada ya kuichalaza bao 1-0. 

NADAL ATWAA TAJI LA MICHUANO YA KOMBE LA ROGER

Mchezaji tenisi nyota Rafael Nadal amefanikiwa kutawadhwa bingwa mpya wa michuano ya Kombe la Rogers baada ya kugaragaza Milos Raonic wa Canada. Nadal mwenye umri wa miaka 27 kutoka Hispania alitumia dakika 68 pekee kushinda mchezo huo kwa 6-2 6-2 na kunyakuwa taji lake la nane kwa mwaka huu. Toka arejee tena uwanjani Februari mwaka huu baada ya kupona majeraha, Nadal amefanikiwa kushinda michezo 48 kati ya 51 aliyocheza na kufanikiwa kushinda taji lake la nane katika michuano ya wazi ya Ufaransa. Kwa upande wa wanawake mwanadada anayeshika namba moja katika orodha za ubora Serena Williams wa Marekani naye alifanikiwa taji la michuano hiyo kwa kumgaragaza Sorana Cirstea wa Romania. Williams mwenye umri wa miaka 31 alihitaji dakika 65 pekee kummaliza mpinzani wake kwa 6-2 6-0 na kunyakuwa taji hilo kwa mara ya tatu.