Monday, December 1, 2014

AVRAM GRANT KOCHA MPYA TIMU YA TAIFA YA GHANA ACHUKUWA MIKOBA YA KWESI APPIAH


KOCHA mpya wa timu ya taifa ya Ghana, Avram Grant ameanza kazi rasmi leo huku akitegemewa kuweka mikakati yake katikati ya wiki. 
Jumatano kocha huyo wa zamani wa Chelsea raia wa Israel anatarajiwa kuzungumza na wanahabari ili kuweka maono na mipango yake kwa soka la Ghana. 
Mkataba rasmi wa kocha huyo unaanza kufanya kazi leo lakini Chama cha Soka cha Ghana kimethibitisha kuwa tayari kocha huyo ameshatua na ataanza rasmi kibarua chake hicho kesho. 
Moja ya kibarua atakachokuwa nacho Grant mwenye umri wa miaka 59 ni kusaidia kujenga shule ya soka ya kitaifa na pia kusaidia mafunzo ya makocha wazawa wan chi hiyo. 
Grant ana wiki sita za kukiandaa kikosi kipya cha Ghana kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika huko Guinea ya Ikweta mapema mwakani.