MENEJA wa klabu ya Liverpool Brendan Rodgers amesema timu hiyo tayari imeshamuofa mkataba mpya kiungo na nahodha wao Steven Gerrard.
Kocha huyo pia alikanusha tetesi za kutoelewana na Gerrard ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Akizungumza kabla ya mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Leicester, Rodgers amesema hakuna ugomvi wowote kati yake na Gerrard na kudai hayo yanayosemwa hayana ukweli wowote.
Kocha huyo aliendelea kudai kuwa Gerrard atapewa muda wa kufikiria ofa hiyo mpya lakini amedai pesa haitakuwa tatizo.
Rodgers amesema amekuwa akifurahia kila dakika kufanya kazi na Gerrard na ni matumaini yake ataendelea kuitumikia klabu hiyo.